Makala

Subira ndefu ya kuzika wafu wa Shakahola

Na BRIAN OCHARO July 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

Miaka miwili iliyopita, walijitokeza mmoja baada ya mwingine kutoa sampuli zao za DNA na hadi sasa wamebaki na vidonda visivyoponyeka huku baadhi yao wakipoteza familia zao nzima.

Walitoa sampuli zao kwa matumaini kuwa miili ya wapendwa wao waliotoweka msituni Kaunti ya Kilifi baada ya mafundisho ya kupotosha ya mhubiri Paul Mackenzie, ingepatikana na kupatiwa mazishi ya heshima.

Lakini miaka miwili baadaye, walichopokea ni kimya. Miili ya wapendwa wao bado iko katika mochari ya Hospitali ya Malindi, ikiwa imewekewa nambari tu.

Bw Suleiman Nyanje Zero ni miongoni mwa familia nyingi ambazo bado hazijapata majibu. Kwao, ahadi ya kupata miili ya wapendwa wao imekuwa maumivu ya kudumu, makali kuliko kifo chenyewe.

Timu ya Taifa Leo ilimtembelea nyumbani kwake Tezo, karibu na Shule ya Msingi ya Mikingirini, Kilifi, takriban dakika 20 kutoka barabara kuu ya Mombasa-Malindi.

Familia yake ya watu wanane sasa imesalia wawili tu. Alimpoteza mkewe, Bi Mbeyu Chombo, mwenye umri wa miaka 42, na watoto wao watano wa umri wa miaka 22, 20, 18, 12 na mmoja na nusu.

‘Nimesalia na mwanangu mkubwa pekee. Alitoroka kutoka Shakahola maisha yalipozidi kuwa magumu. Nilikuwa na bahati. Ningepoteza kila mtu,’ anasema.

Hajazika mpendwa yeyote na hajui walipo. Anaishi peke yake kwani mwanawe yuko mbali kutafuta riziki.

‘Tulitoa DNA mwaka wa 2023, lakini bado sijapokea majibu. Sijui kama wako mochari au bado wamezikwa msituni,’ anasema.

Simu pekee aliyopokea kutoka kwa wachunguzi ilikuwa ya kumuita kutoa ushahidi mahakamani.

‘Serikali ilihitaji tu ushahidi wangu lakini haijafanya lolote kunisaidia kupata familia yangu au kuwazika kama wamefariki. Tangu nilipoitwa kutoa ushahidi dhidi ya Mackenzie, hakuna aliyezungumza nami tena,’ anasema huku akijizuia kulia.

Aliwaona wapendwa wake mara ya mwisho mwaka wa 2019, mkewe alipojiunga na kanisa la Good News International na kuwa karibu na Mackenzie.

‘Alikuwa akiwatunza watoto wa Mackenzie na kulipwa kidogo. Sikumzuia kwenda kanisani kwani nilidhani mambo yalikuwa sawa,’ asema.

Hofu ilianza alipoingia msituni na watoto wote. Alijaribu kuwatafuta bila mafanikio hadi alipoona kwenye habari kuwa miili ilikuwa ikifukuliwa Shakahola.

‘Kwa sababu serikali haitoi taarifa, sina wa kumuuliza kuhusu familia yangu. Nahisi wamefariki maana wangekuwa wamerudi. Mke wangu si miongoni mwa waliokamatwa,’ asema.

Anaongeza, ‘Nataka kujua walipo. Hatuwezi kuteseka mara mbili – kupoteza na kusubiri bila kikomo.’

Ms Zueni Ali anasema baba yake wa kambo, Stephen Shoboi, alifariki akisubiri mwili wa mamake, Bi Jumwa Chea, aliyepotelea msituni. Alituachia maagizo kuwa mamake azikwe katika shamba la wazazi wake iwapo mwili wake utapatikana.

Yeye na nduguye walitoa sampuli za DNA lakini bado hawajapokea majibu. Wote walikuwa wamejiunga na Mackenzie kabla yake kutoroka na kutoa ushahidi mahakamani.

Katika kijiji cha Kamale, zaidi ya kilomita 150 kutoka mji wa Malindi, tulikutana na Bw Titus Ngonyo Gandi, aliyepoteza wanawe wawili, wake zao na wajukuu.

‘Nimechoka kuzika watu awamu kwa awamu. Nataka nizike wote kwa pamoja nipate amani. Tayari nimezika wanne tarehe tofauti; watatu wanasalia. Kila mazishi hufungua jeraha jipya,’ anasema.

‘Mwaka jana DCI waliniambia kuwa mwili wa mwanangu Isaack Ngala ulitambuliwa. Waliniambia utatolewa ndani ya wiki mbili. Bado nasubiri hadi leo,’ asema.

Hali hiyo ni sawa na ya Bw Gerishon Musau, aliyempoteza binti yake Ruth Minoo. Alitoa DNA Mei 2023 na bado hajapata jibu.

‘Nataka kujua yuko wapi. Kama amekufa, basi tuzike. Tunaomba serikali ichukue hatua haraka,’ asema.

Jimmy Mganga anatafuta baba yake Moses Kahindi, mama yake Joyce Kachi, na ndugu zake watatu ambao wote hawajulikani walipo.

‘Hadi sasa, sijapokea majibu. Kila nikiuliza naambiwa hakuna vifaa vya kushughulikia sampuli,’ anasema kwa uchungu.

Kulingana na rekodi za serikali, ni miili 72 tu kati ya zaidi ya 450 iliyofukuliwa imetambuliwa, na 34 pekee imezikwa.

Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu (KNCHR) inakadiria kuwa zaidi ya watu 600 bado hawajulikani walipo, na chini ya asilimia 10 ya waathiriwa wa Shakahola wamerejeshwa kwa familia zao.

Katika mochari ya Malindi, shughuli zinaendelea, lakini si za kuondoa miili ya Shakahola. Wafanyakazi wanasema miili ya mwisho kuchukuliwa ilikuwa mwaka jana. Miili zaidi ya 400 bado ipo, mingi ikiwa haijatambuliwa.

‘Miili hii bado iko hapa. Tunahangaika nayo hadi leo,’ alisema mfanyakazi mmoja kwa ombi la kutotajwa jina.