Rais Biya, 92, atokwa kijasho kuvutia vijana kwenye kampeni ya kusalia mamlakani
YAOUNDE, CAMEROON
JUHUDI za Rais Paul Biya, 92, kuwavutia vijana kabla ya uchaguzi wa Oktoba huenda zinaambulia patupu, wachanganuzi wamesema.
Hata kabla ya Biya ambaye ni rais mkongwe zaidi duniani kuthibitisha atawania muhula wa nane mamlakani, akaunti zake kwenye mitandao ya kijamii zilikuwa ithbati tosha kwa wataalamu.
Kufikia wakati alipotangaza rasmi kwamba angegombea kuchaguliwa kwa mara nyingine kuwa rais wa Cameroon wiki iliyopita, alikuwa tayari ameanza kuboresha uwepo wake mitandaoni kwa miezi kadhaa.
Jumbe zake za kila siku kwenye mitandao ya kijamii ya Facebook na X ziliashiria taswira tofauti kabisa na hali yake ya kawaida.
Hata hivyo, juhudi za Biya kuvutia umaarufu kutoka kwa raia wachanga kabla ya uchaguzi huenda zinagonga mwamba kwa mujibu wa wachanganuzi.
“Cameroon ina watumiaji mitandao zaidi ya 5.4 milioni lakini asilimia 95 ya vijana hutegemea WhatsApp – mtandao wa kijamii ambamo mawasiliano ya urais ni finyu,” asema mkurugenzi wa kampuni ya Media Intelligence Sarl na mwandishi wa Ripoti ya Cameroon 2024 Multimedia Audience, Rostant Tane.
Kikwazo kingine ni uhalisia ambapo mhadhiri wa sayansi ya mawasiliano, Hervé Tiwa, anafafanua kwamba “Watu wengi wanajua si Paul Biya – anayeandika mwenyewe – hali inayozua pengo na kupunguza Imani.”
“Mawasiliano yao yamesalia kuwa ya kutoka ngazi za juu chini pasipo ushirikishaji halisi – maoni yanapuuzwa au kufutwa, kukosa majibu ya moja kwa moja…hali inayoibua taswira ya mikakati ya kubandikia zaidi kuliko ushirikishaji.”
Sehemu kubwa ya raia Cameroon ni vijana ambapo zaidi ya asilimia 60 wako chini ya umri wa miaka 25 huku zaidi ya nusu ya wapiga kura wakiwa chini ya umri wa miaka 30 kumaanisha wanaweza kuamua matokeo ya uchaguzi.
“Mawasiliano ya kisiasa ni sharti yazingatie demokrasia na uwazi, na si kutumika tu kama wenzo wa mauzo,” anaeleza mtaalamu wa mawasiliano, 27, Ulrich Donfack.
Ukosefu wa ajira umekithiri nchini ambapo hata vijana waliofuzu kwa shahada kadhaa za digrii kutoka vyuo vikuu wanahangaika kusaka kazi.
Vilevile, ufisadi na usalama ni masuala nyeti.
Badala ya kuzingatia masuala hayo, jumbe nyingi zinazochapishwa kwenye akaunti za Biya mitandaoni zinasisitiza rekodi yake akiwa mamlakani kwa miaka 43 – kipindi ambapo sehemu kubwa ya wananchi hawakuwa wamezaliwa.
Kulingana na mtaalamu wa mikakati ya mawasiliano, Aristide Mabatto, kikosi cha Biya sasa kinachapisha taarifa kwa Kifaransa na Kiingereza kutoka kwa hotuba zaidi ya 300 ambazo rais alitoa miongo iliyopita.
Mfano mmoja ni hotuba ya mwaka 2,000 akisuta watu wanaowazomea wengine ila wanakosa kuhubiri kwa vitendo, iliyochapishwa siku mbili tu baada ya wandani wake Biya kwa miaka mingi walikosoa utawala wake na kumtema.
Biya alikosa kuonekana hadharani kwa zaidi ya wiki sita mwaka uliopita hali iliyosababisha tetesi kuhusu afya yake na uvumi kuwa amekufa.
Wafuasi wake wamesifu juhudi hizi mpya huku idhaa za kitaifa kama vile Cameroon Tribune ikiangazia mikakati ya kidijitali ya Biya kama ishara ya uchanga na uongozi.