Jamvi La Siasa

Sababu za Raila kumtetea Sifuna kwa kukosoa Ruto

Na WAANDISHI WETU July 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

Kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kwa mara nyingine amemtetea Katibu Mkuu wa chama hicho, Edwin Sifuna, kwa kukosoa vikali makubaliano kati ya chama chake na Rais William Ruto.

Katika mahojiano ya televisheni Jumanne usiku, Bw Sifuna alizidisha mashambulizi kwa kusema kuwa mkataba wa makubaliano kati ya ODM na UDA “umekufa” kwa sababu upande wa Rais Ruto haujatimiza masharti ya makubaliano hayo.

Kauli yake kali ilijiri siku tatu baada ya Bw Odinga kuthibitisha kuwa ataendelea kushirikiana na Dkt Ruto hadi mwaka wa 2027. Waziri wa Kawi, Bw Opiyo Wandayi, naye aliongeza kuwa ODM itashikilia mkataba huo hadi 2032, hali iliyozidisha mkanganyiko miongoni mwa viongozi na wafuasi wa chama hicho.

Hatua Bw Sifuna ya kukosoa Serikali  Jumuishi ilishutumiwa vikali na baadhi ya wafuasi na viongozi wakuu wa ODM ambao wanahisi kwamba anampinga Bw Odinga na kukiuka maamuzi ya chama.

Hata hivyo, jana katika kongamano la wajumbe wa ODM kaunti ya Kakamega, Bw Odinga alimtetea tena Bw Sifuna, akisisitiza kuwa bado ndiye msemaji rasmi wa chama na ana haki ya kutoa maoni yake.

“Sifuna ana haki ya kuzungumza. Kama hutakubaliana naye, toa maoni yako. Hiyo ndiyo demokrasia. Hata mimi, mtu akiwa na hisia kwamba nimekosea, anapaswa kuniambia. Kama ODM itasema nimechoka na niende Bondo, watanieleza. Lakini lazima tulinde na kukuza demokrasia ndani ya chama,” alisema Bw Odinga.

Alisisitiza kuwa ODM ni chama cha kidemokrasia ambacho kinapaswa kuvumilia tofauti za maoni.

Alipendekeza kuwa wale walio na matatizo na Katibu Mkuu watumie njia rasmi za chama kama Baraza Kuu ya Kitaifa (NEC) na Kamati Kuu ya Kitaifa badala ya kuzungumza kupitia vyombo vya habari.

“Kutakuwa na tofauti za maoni, lakini lazima tulinde haki ya kila mwanachama kusema. Kama hukubaliani na Sifuna, usijibu kwenye vyombo vya habari. Tumia mifumo ya chama kushughulikia suala hilo,” alisema Bw Odinga.

Alibainisha kuwa ni katika vikao hivyo ambapo wanachama hujadili na kutoa maoni yao, kisha uamuzi wa pamoja unaafikiwa na kutangazwa na Katibu Mkuu.

“Katibu Mkuu Sifuna ndiye anahutubia vyombo vya habari kuhusu maamuzi ya chama. Yeye ndiye msemaji rasmi wa ODM. Lakini baada ya mazungumzo na maelewano, msimamo wa chama ni wa wote,” alieleza Bw Odinga.

Kuhusu suala la mkataba, Bw Odinga alieleza kuwa kuna maeneo ambayo serikali haijatekeleza kama walivyokubaliana Februari.

“Ni Sifuna aliyeandaa makubaliano hayo na UDA. Niliposoma, nilisaini kama hatua ya muda ya kushughulikia changamoto kubwa zinazowakumba Wakenya. Lakini utekelezaji wake umekuwa changamoto. Kwa mfano, hatuwezi kukubali matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji. Polisi hawapaswi kutumia risasi halisi,” alisema Bw Odinga.

Aliongeza kuwa walikubaliana pia kuhusu fidia kwa waathiriwa wa maandamano na walioumia.

“Tulitia saini mkataba na UDA. Tutaurejelea, tuone kilichotekelezwa na kisichotekelezwa, kisha tuamue hatua inayofuata. Yale tuliyokubaliana na Rais Ruto lazima yatekelezwe,” alisisitiza Bw Odinga.

Wakati huo huo, viongozi wa Magharibi waliokuwepo katika mkutano huo walimtetea Bw Sifuna.

“Mkilaumu Sifuna, mnanilaumu mimi. Mimi ndiye niliyempa ruhusa ya kuzungumza hivyo kwenye runinga. Mkisema aondoke, basi nami pia nitajiondoa. Hakuna mahali tumeketi na kumuunga mkono yeyote kwa urais. Raila ndiye atakayetupa mwelekeo,” alisema Seneta wa Vihiga, Bw Osotsi.

Alisema ODM itawasilisha wagombea kuanzia MCA hadi urais mwaka wa 2027.

Katibu Mkuu wa COTU, Francis Atwoli, ambaye amekuwa mkosoaji wa Sifuna, alibadilika na kusema sasa anaelewa kuwa Sifuna alikuwa sahihi na anaungwa mkono na wafuasi.

“Wakati wa KANU, Katibu Mkuu Joseph Kamotho hangesema jambo ambalo Moi hajui. Nilipomsikia Sifuna akiongea, sikuwa nimeelewa hoja zake. Lakini sasa nimeelewa kwamba alikuwa sahihi na alikuwa na uungwaji mkono,” alisema Bw Atwoli.

Gavana wa Kakamega Fernandes Barasa alisema ODM iko serikalini hadi 2027, ambapo Bw Odinga atawapa mwelekeo.

Huko Muhoroni, Kisumu, wakati wa shughuli ya kuwawezesha wananchi, Mwenyekiti wa ODM na Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga alisema kauli za Sifuna ni za kibinafsi na hazionyeshi msimamo wa chama.

“Kama mwenyekiti wa chama, nataka kuwa wazi. Bado tuko ndani ya makubaliano hayo. Ni Raila Odinga pekee anayeweza kuamua kujiondoa,” alisema Bi Wanga.

Alionya dhidi ya kauli zinazoweza kugawa au kuyumbisha mshikamano wa chama.

“Mtu akisema mkataba umekufa, hafanyi hivyo kwa niaba ya ODM. Hatutaki kufuata njia ya Wamunyoro,” aliongeza, akimrejelea Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Mwakilishi wa Wanawake Kaunti ya Kisumu Ruth Odinga pamoja na viongozi wengine wa juu wa ODM waliounga mkono msimamo wa Bi Wanga.