Maoni

IEBC ishirikishe wadau wote katika maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2027

Na BENSON MATHEKA July 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KUUNDWA upya kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, ­IEBC, kulifungua ukurasa mpya wa matumaini katika maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Hili ni jambo la kupongezwa, lakini sasa kazi ya kweli inaanza. Ili uchaguzi huo uwe wa haki, huru na wa kuaminika, IEBC inapaswa kushirikisha wadau wote kikamilifu katika kila hatua ya maandalizi.

Kwa miaka mingi, changamoto kubwa katika uchaguzi Kenya imekuwa ni ukosefu wa imani kwa IEBC, hali inayochochewa na hisia kuwa baadhi ya maamuzi hufanywa kwa siri au kwa upendeleo.

Ili kurejesha imani hiyo, tume hii haina budi kufungua milango ya ushirikiano na wadau wote –vyama vya siasa, asasi za kiraia, viongozi wa kidini, mashirika ya kimataifa, na wananchi wa kawaida.

Ni kwa msingi huu kwamba IEBC inapaswa kuanza sasa – bila kuchelewa – mchakato wa mashauriano ya wazi na ya mara kwa mara na wadau wote.

Kalenda ya uchaguzi, teknolojia zitakazotumika, uwezekano wa marekebisho ya sheria za uchaguzi, na mambo mengine ya msingi, yote haya yanahitaji mjadala wa pamoja.

Watu wanahitaji kuelezwa, kuelimishwa na kushirikishwa kikamilifu katika kila hatua. Pia, tume hii ina jukumu la kuhakikisha kuwa wananchi wanapata elimu ya kutosha kuhusu haki na wajibu wao kama wapiga kura.

Elimu hii isiwe ya muda wa mwisho, bali ianze sasa kwa kutumia lugha rahisi, njia shirikishi na kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali yaliyo mstari wa mbele katika kutetea haki za kidemokrasia.Wakati umefika kwa IEBC kujivua kabisa taswira ya chombo kinachofanya kazi kwa usiri, mbali na wananchi.

Ni lazima tume hii ijenge utamaduni mpya wa kusikiliza, kushirikisha na kushirikiana. Kwa kufanya hivyo, itaweza kurejesha imani ya wananchi na kuhakikisha kuwa uchaguzi wa 2027 hautakuwa chanzo cha migawanyiko bali utaleta umoja kwa maendelezo ya taifa.

Ili iweze kufaulu, IEBC haifai kutumiwa au kuonekana kutumiwa na upande au kupendelea upande mmoja. Ishirikishe wadau wote, itoe taarifa kwa uwazi, na kuweka maandalizi yote wazi kwa Wakenya.