Jamvi La Siasa

Munyi aliamini siasa ni huduma si kujitajirisha

Na KWA HISANI YA KENYA YEAR BOOK July 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KAMWITHI Munyi hakuwa mtu wa kawaida katika siasa za Kenya. Kwa wengi waliomtazama katika mikutano ya hadhara iliyohudhuriwa na Rais Daniel arap Moi, alijulikana kwa tabia yake ya kipekee – tabasamu lisiloisha, suti za rangi mbalimbali, na tabia ya kukubali kila kauli ya rais kwa kutikisa kichwa.

Lakini mbali na muonekano wake wa kipekee, Munyi alikuwa mwanasiasa mwenye mizizi imara.Aliweka historia mwaka wa 1988 kwa kupata kura nyingi zaidi za ubunge nchini, alipozoa kura 29,696 dhidi ya mpinzani wake aliyepata kura 13,016.

Hii ilikuwa ni baada ya kuwakilisha eneobunge la Embu Mashariki tangu 1969, alipochaguliwa bila kupingwa.Munyi alizaliwa Septemba 1 1937. Akiwa kijana, alisomea Cairo, Misri, katika Chuo Kikuu cha Amerika, akajifunza Sayansi ya Siasa na Diplomasia.

Akiwa huko, alijiunga na wanaharakati wa uhuru kama Henry Gathigira, akiwasaidia wanafunzi wa Kenya kupata masomo nje ya nchi, licha ya vikwazo vya mkoloni.Alitajwa na Jaramogi Oginga Odinga katika kitabu chake Not Yet Uhuru kama mmoja wa watu waliokuwa mstari wa mbele katika harakati za ukombozi.

Baada ya kurejea Kenya mwaka 1962, Munyi hakutafuta ajira bali alijiingiza moja kwa moja katika siasa. Alikuwa mwenyekiti wa tawi la KANU Embu kuanzia 1962 hadi 1976, alipoondolewa na mpinzani wake mkuu, Waziri wa zamani Jeremiah Nyagah. Hii ilizua mvutano mkubwa wa kisiasa katika eneo hilo, haswa kati ya jamii mbili kuu – Aembu na Ambeere.

Wakati Aembu walimiliki ardhi yenye rutuba, Mbeere waliishi maeneo kame, na mara nyingi walihisi kudharauliwa. Munyi, ingawa alikuwa Embu, alipata uungwaji mkono kutoka kwa baadhi ya Ambeere kutokana na utu wake na juhudi za maendeleo.

Wakati wa urais wa Moi, Munyi alitumia nafasi yake kushirikiana na kamati za maendeleo za wilaya (DDC) kuanzisha miradi muhimu kama daraja la Irira, ambalo liliunganisha maeneo ya Evurori na Nthawa.

Alifanikiwa pia kushawishi utafiti wa aina ya mahindi ya Katumani kwa ardhi kame ya Mbeere kupitia KARI.Uwezo wake wa kuwasiliana na wananchi ulimfanya apendwe zaidi, hasa alipokuwa akiwakosoa viongozi kama Nyagah kwa “kutowajali wananchi wa kawaida.”

Baada ya kupoteza kiti cha ubunge mwaka 1983, Munyi alirudi kwa kishindo mwaka 1988 katika eneo jipya la Runyenjes. Lakini mwaka 1992, wakati chama cha KANU kilipopoteza ushawishi Mlima Kenya, hakufanikiwa kutetea kiti chake. Hata hivyo, uaminifu wake kwa Moi ulimwezesha kuteuliwa kuwa Waziri wa Ushirika na Maendeleo.

Moi alitambua uaminifu wa viongozi waliobaki ndani ya KANU licha ya mawimbi ya upinzani. Munyi alikuwa mmoja wa wanasiasa waliobaki waaminifu kwa chama hicho cha uhuru.Munyi alijulikana kwa kuvaa saa mbili za bei ghali kwa mkono mmoja baadhi ya watu wakisema alikuwa mpenda anasa.

Licha ya hadhi yake, alijulikana kuwa mtu wa watu, aliyepokea wananchi nyumbani kwake Kyeni na kusikiliza matatizo yao kwa moyo wa upendo.

Hata hivyo, matamshi yake ya 1994 kuhusu “wageni” hususan Wakikuyu waliokuwa wakiunga mkono upinzani Embu, yalizua hasira miongoni mwa viongozi wa kidini.

Askofu Moses Njue wa CPK alieleza kuwa kauli hizo zilikuwa hatari na zenye kugawanya watu wa jamii moja.Tofauti na wanasiasa wengi, maisha binafsi ya Munyi hayakujulikana sana.

Alifariki mwaka 2006, na wengi walimkumbuka kama kiongozi wa kweli, aliyepigania maendeleo, aliyependa wananchi wake, na aliyeamini kuwa siasa ni njia ya kutumikia watu, si kujinufaisha binafsi.