Habari

Hofu askari gongo wakiuawa na kung’olewa ulimi Kakamega

Na SHABAN MAKOKHA July 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

POLISI wameanza kumsaka mwanaume ambaye amekuwa akihusishwa na mauaji yanayowalenga walinzi wa usiku Kakamega kisha kutumia sehemu za miili yao kufanya matambiko.

Kwa kipindi cha wiki sita zilizopita, zaidi ya askari gongo saba wameuawa mjini Kakamega na kuzua taharuki kubwa mjini humo.

Mauaji hayo yamesababisha wafanyabiashara kufunga biashara zao mapema mno baadhi kufikia saa mbili usiku.

Walinzi nao wameingiwa na wasiwasi kuhusu hatima ya maisha yao huku wakidai wanalengwa na wahalifu hao.

Kinachosikitisha ni kwamba mauaji hayo yamekuwa yakifuata mkondo fulani ambapo ulimi wa aliyeuawa hukatwa na kutolewa.

Kinachoshangaza zaidi ni kwamba hakuna chochote kinachoibwa kutoka kwa walinzi hao.

Ndani ya mwezi mmoja, watu saba wamekufa ndani na viungani mwa Kakamega lakini hakuna mshukiwa yeyote ambaye amekamatwa.

Mauaji ya hivi karibuni ni karibu na Chuo Kikuu cha Masinde Muliro na Kanisa la Kiadventista la Maraba, matukio yakifanyika saa 10 asubuhi.

Kanda ya CCTV kutoka kwa duka moja la vipuri Lurambi ilionyesha kijana akiwa gizani akimvamia askari gongo na kumuua ndani ya dakika sita.

“Mvamizi huyo hataki kumwona yeyote anayejiita mlinzi. Lengo lake ni askari gongo si watu wengine,” akasema mmiliki wa duka hilo Jane Odongo.

Kilichosikitisha ni kuwa mlinzi aliyeuawa alikuwa ndiyo ametwaa majukumu hayo baada ya mwenzake kuvamiwa siku mbili zilizotangulia.

Kamanda wa Polisi wa Kakamega ya Kati Vincent Cherutich alifichua kuwa mshukiwa huonekana akiwa amebeba mfuko wa plastiki ambao yeye huweka chini kabla yeye kutekeleza uvamizi.

Akishamvamia anajificha nyuma ya lori lililoegeshwa kisha anajificha gizani.

Mlinzi huyo alipatikana asubuhi akiwa amevunjika meno na kukimbizwa hadi Hospitali ya Kaunti ya Kakamega na akafa akipokea matibabu baada ya kuhamishwa hadi Hospitali ya Kisumu.

Pius Ngwete, 55, naye alipatikana ameuawa nje ya Kanisa la Maraba SDA akiwa na majeraha mabaya kichwani.

Polisi walithibitisha hakuna kilichoibwa kutoka kwake na hata kanisa lenyewe hakuna kilichopotea.

Mapema mwezi huu zaidi ya walinzi watatu waliuawa karibu na Kituo cha Polisi cha Lurambi. Mmoja alikufa papo hapo, wawili wakifa siku mbili baadaye wakipokea matibabu.