Hitilafu ya treni yawaharibia maelfu mipango ya Valentino
Na GEOFFREY ANENE
ILIKUWA Valentino ya taabu baada ya abiria wanaotumia treni linalohudumu katika barabara ya Ruiru hadi jijini Nairobi kutatizika Alhamisi asubuhi na kuchelewa kwa saa nzima kufika katikati ya jiji la Nairobi baada ya treni hilo kukwama katika eneo la Kariobangi South na Makadara.
Treni hilo, ambalo hutumiwa na maelfu ya abiria kila siku, lilikwama katika shule ya Soul Mercy Education Centre, hatua chache kabla ya kufika steji ya Kariobangi South.
Huwa linasimama steji ya Kariobangi South almaarufu KCC saa moja na dakika kumi asubuhi likielekea katikati mwa jiji la Nairobi.
Hata hivyo, lilizima katika shule ya Soul Mercy saa moja na dakika kumi. Dereva wa treni hiyo aliitisha injini ingine kutoka kituo cha Makadara.
Karibu nusu ya abiria waliamua kutafuta usafiri wa magari ya matatu kufika walikokuwa wakienda. Nauli ya treni huwa Sh40. Walioamua kuabiri magari walilazimika kulipa Sh70, nauli ambayo magari yanayohudumu barabara ya Kariobangi South hadi katikati mwa jiji hulipisha.
Injini ya treni ilifika zaidi ya dakika 30 baadaye na baada ya dakika saba, safari ikaendelea bila tatizo lolote. Garimoshi lilisimama katika kituo cha KCC dakika moja likipata abiria wachache walioamua kusubiri walipoona injini ingine ikiwasili.
Safari iliendelea vyema, huku garimoshi hilo likishusha na kubeba abiria wengine katika stegi ya Mutindwa inayopana ana barabara ya magari ya Outering Road saa mbili na dakika moja kwa dakika mbili.
Lilishusha abiria wengine katika kituo cha Makadara kinachopakana na barabara ya Jogoo Road dakika nane baadaye. Watu wengi hushuka katika kituo cha Makadara wakienda kufanya kazi katika eneo la Industrial Area.
Matatizo yaliyokumba injini ya kwanza yalijitokeza tena Makadara, treni likikwama licha ya kuvutwa na injini mbili. Baadhi ya abiria waliamua kikimbilia garimoshi lingine lililokuwa limefika eneo hilo likielekea mjini.
Treni hilo, hata hivyo, liliwaka tena na baada ya kunguruma, safari ikaendelea saa mbili na dakika 33 na kufika stegi kuu saa tatu kasorobo.