Kimataifa

Raia wa Gaza wakeketwa na njaa Israel ikitwikwa lawama za ukatili

Na REUTERS July 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

GENEVA, UMOJA WA MATAIFA (UN)

SHIRIKA moja la Kimataifa la Kupambana na Njaa, limeonya kuwa hali katika Ukanda wa Gaza sasa imefikia kiwango hatari wengi wakiendelea kufa kwa kukosa chakula.

Hali hii hatari inatokea wakati ambapo idadi ya waliokufa tangu Israel ivamie Gaza mnamo Oktoba 7, 2023 imefika watu 60,000 kwa mujibu wa Wizara ya Afya Gaza.

Shirika linalohusika na utoshelevu na usalama wa chakula duniani maarufu kama IPC limesema kuwa njaa ambayo inakeketa raia wa Gaza inafikia kiwango cha kutajwa kama janga la njaa.

IPC ilisema kuwa wakati umefika ambapo Israel na Amerika lazima zishinikizwe ili ziruhusu chakula na misaada mingine iwafikie raia wa Gaza bila kudhibitiwa.

“Kuna ushahidi kuwa kuna njaa, utapiamlo na ugonjwa na hizi zote zimechangia njaa kali sana,” ikasema IPC.

Licha ya tangazo na shinikizo za IPC bado haijafahamiki iwapo Israel italegeza kamba na kuruhusu misaada iwafikie raia milioni 2.1 wa Gaza.

“Tangu Israel ianze kuweka vikwazo, ni chini ya asilimia 50 ya msaada pekee imeingizwa Gaza,” ikasema IPC.

Ross Smith kutoka Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) naye alisema watu 470,000 wameathirika na njaa, 90,000 wakiwa wanawake na watoto ambao wanahitaji vyakula vyenye madini ili kujiokoa.

Kwa mujibu wa wizara ya afya Gaza watu 147 wameaga dunia kutokana na njaa wakiwemo watoto 88 ndani ya wiki chache zilizopita.

Israel imekashifiwa vibaya baada ya picha ya watoto ambao wamedhoofika kusambaa mitandaoni.

Jumapili ilibidi Israel isitishe vita katika baadhi ya maeneo ambayo yameathirika vibaya ili kupisha msaada utolewe kwa raia.

IPC imesema kwa sasa wanaoishi Gaza wanahitaji tani 62,000 ya vyakula kila mwezi lakini inasikitisha mnamo Mei Israel iliruhusu tu tani 19,900 kisha Juni tani 37,800.