Habari za Kitaifa

Hisia Uhuru na Ruto wanasuka kitu baada ya kukutana Ikulu

Na JUSTUS OCHIENG, GEORGE ODIWUOR August 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 3

Mkutano wa Rais William Ruto na mtangulizi wake Uhuru Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi Ijumaa pamoja na matembezi yao pamoja umeibua hisia mseto huku ukizua mjadala kuhusu maana yake kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Rais Ruto alimtaja Kenyatta kama ‘rafiki yangu wa dhati’ alipochapisha picha za mkutano huo na ziara ya kibinafsi Ikulu ya Nairobi ambayo Kenyatta alitumia kama makazi rasmi kwa miaka 10. Picha hizo zilifuatia zile zilizosambazwa awali na washirika wa Ruto, zikionyesha urafiki wao wa awali wakati wa muhula wa kwanza wa utawala wa Jubilee.

Ingawa ziara hiyo ya Ikulu ilifuatia mazungumzo ya amani kuhusu Congo na ilionekana ya kawaida, wachambuzi wa siasa wanasema huenda ilinuiwa kutoa ujumbe zaidi.

Viongozi hao wawili, ambao hapo awali walikuwa washirika wa karibu kabla ya kutofautiana kuelekea uchaguzi wa 2022 – ambapo Kenyatta alimuunga mkono Raila Odinga – bado hawakubaliani kuhusu mwelekeo wa uongozi wa kisiasa nchini, huku Kenyatta akidaiwa kumuidhinisha aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i kumng’oa Ruto madarakani kupitia uchaguzi 2027.

Wandani kutoka pande zote mbili wanasema bado kuna mvutano, huku wengine wakidai Kenyatta anasaka mkakati wa kupanga urithi wa urais 2027 licha ya kujiondoa hadharani kwenye siasa.

Kuonekana kwake Ikulu, wanasema, huenda ni sehemu ya mpango mpana wa kurejesha ushawishi wake katika mazingira yanayobadilika ya kisiasa.

‘Hakukuwa na jambo kubwa. Tunajua kuwa jamii ya kimataifa inataka Uhuru ashikilie nafasi ya kikanda kuhusu amani, lakini ina wasiwasi na uhusiano wake na Rais Ruto,’ afisa mmoja wa Ikulu aliambia Taifa Jumapili.

‘Kwa kuwa ndiye aliyeomba kutembelea Ikulu ili kuzoea mabadiliko mapya, tunaamini alitaka kujionyesha kwa jamii ya kimataifa kuwa hana kinyongo dhidi ya mrithi wake na yuko tayari kwa jukumu lolote la usalama wa kikanda.’

Lakini Seneta wa Nandi, Samson Cherargei, alionekana kufurahia ziara hiyo akisema ni ishara ya kukubalika kwa Ruto kitaifa na dalili kwamba atashinda 2027.

‘Kuwepo kwa Uhuru Ikulu na Rais Ruto kumechanganya wanaoeneza ukabila kwa sababu hawataki Kenya jumuishi, iliyoungana. Hii pia ni thibitisho kuwa ‘tutam’ ni wazi kabisa kwa serikali ya Ruto. Uchaguzi wa 2027 utakuwa kama hafla ya kumvika taji Rais; wapinzani wangoje 2032,’ alisema Cherargei.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kitaifa wa Chama cha Jubilee Torome Saitoti alikanusha dhana kwamba ziara ya Kenyatta ilikuwa ya kisiasa.

‘Alikuwa na mkutano tofauti kabisa na watu wasitafute maana nyingine,’ alisema Saitoti.

Simu, jumbe za maandishi na WhatsApp kwa Naibu Mwenyekiti wa Jubilee David Murathe na Katibu Mkuu Jeremiah Kioni hazikujibiwa.

Chama cha DCP cha Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua kilipuuza tukio hilo, Naibu Kiongozi wake Cleophas Malala akisema ni ‘michezo wa macho tu’.

‘Tunajua Uhuru alikuwa Ikulu kwa sababu ya juhudi za amani Congo na kama Rais wa zamani ana haki ya kutembelea Ikulu. Lakini hatutishiki na mambo kama haya ya kuonyesha sura tu. Mkutano huo hauwezi kuokoa Ruto akose kuwa rais wa muhula mmoja tu,’ alisema Malala.

Profesa Gitile Naituli wa Chuo Kikuu cha Multimedia alikejeli tukio hilo.

‘Uhuru alikuwa maarufu sana kwa kuchukiwa. Watu hawakumpenda. Alipanga mgogoro wa uongo na Ruto ili amzuie Raila,’ alisema Prof Naituli.

‘Kuanzia ICC hadi mradi wa reli ya SGR, walifanya mambo pamoja chini ya Jubilee. Hii ni Jubilee Sehemu ya Pili.’.

Baada ya uchaguzi wa 2022, Raila na Uhuru wamekuwa wakifuata njia tofauti kisiasa – Odinga akikaribiana na Ruto kupitia mazungumzo ya pande mbili, huku Kenyatta akiwa kimya kwa muda hadi hivi majuzi alipoibuka tena katikati ya tetesi za miungano mipya.

Odinga mwenyewe, kwenye mahojiano ya hivi majuzi, alikanusha madai kuwa alinufaika kisiasa kutokana na handisheki yake na Kenyatta.

‘Hakuna mtu wangu aliyeteuliwa serikalini. Nilipewa nini? Hakuna kitu,’ alisema Odinga.

Alieleza kuwa msaada wa Kenyatta ulikuwa wa kisiasa na wa wazi – si wa ahadi ya nyadhifa.

‘Uhuru alikuwa anaondoka. Alisema angenisaidia, na akafanya hivyo. Hilo ndilo jambo pekee lililotokea. Sasa, nilikubaliana naye vipi?’ alisema Odinga.

Mjadala kuhusu ziara ya UhuRuto Ikulu uliendelea kushika kasi katika mitandao ya kijamii.

Mchambuzi wa siasa na wakili Wahome Thuku, mshirika wa Gachagua, alitilia shaka dhana kuwa ilikuwa ziara ya kawaida.

‘Mambo mawili. Kwanza, usiniambie tangu Septemba 2022, Uhuru Kenyatta – ambaye anaishi karibu na Ikulu – hajawahi kuwa pale. Kumbuka Ruto alitembelea Ichaweri. Pia, kuna madai ya hivi majuzi kuwa Raila alizungumza na Uhuru kabla ya handisheki yake na Ruto,’ alisema Thuku.

Kwa ucheshi, aliongeza: ‘Pili, kwenye picha hizo, hawa wawili hawakuwa wakizungumzia vita vya Congo. Bila shaka walikuwa wakijadili siasa za Mlima Kenya na mpangilio wa 2027.’

TAFSIRI: BENSON MATHEKA