Habari Mseto

Polisi wanasa kilo 265 za nyama ya punda iliyoharibika Embu na kuacha wakazi na hofu

Na GEORGE MUNENE August 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

POLISI, wikendi, walitwaa kilo 265 za nyama ya punda ambayo ilidaiwa kuharibika, katika eneo la Mbeere, Kaunti ya Embu.

Wakati wa operesheni hiyo, mshukiwa mmoja alinyakwa na kufungiwa kwenye Kituo cha Polisi cha Siakago.

Maafisa wa usalama wakitegemea taarifa za kijasusi, walifahamishwa kuwa nyama hiyo ilikuwa ikisafirishwa mjini Embu kutoka kijiji cha Kathangutari na washukiwa wawili.

Polisi walimnyaka mshukiwa mmoja huku mwengine akitoroka. Mshukiwa aliyenyakwa atafikishwa mahakamani Jumatatu.

Polisi waliwaonya wakazi dhidi ya kununua nyama ambayo haijakaguliwa na hawajui imetoka wapi.

Gari lililokuwa likisafirisha nyama hiyo iliyokuwa imewekwa kwenye magunia lilisimamishwa na polisi likielekea Embu.

Pia ngozi ya punda ilipatikana wakati wa operesheni hiyo.

Tukio hilo linajiri baada ya polisi kufumania nyama ya punda 20 waliokuwa wamechinjwa katika boma moja eneobunge la Runyenjes mnamo Desemba mwaka jana.

Miezi miwili iliyopita, punda 31 walipatikana wamechinjwa kwenye boma moja eneo la Makutano, eneobunge la Mbeere Kusini.

Tukio hilo liliibua hofu kuwa huenda wakazi wamekuwa wakila nyama ya punda bila kujua.

“Wakazi wanafaa wachukue tahadhari ili wazuie kuyahatarisha maisha yao,” mmoja wa maafisa wa polisi akasema.