Trump apanga kuwarusha wahalifu sugu nchi fukara
WASHINGTON, AMERIKA
RAIS Donald Trump amesema baadhi ya wahalifu sugu wanahitaji kusafirishwa kimabavu hadi nchi maskini kwa sababu hata nchi zao wanakotoka hazitawakubali.
Hata hivyo, udadisi wa visa vya hivi karibuni unaashiria wanaume wasiozidi watano waliotishiwa adhabu hiyo walirudishwa mataifa yao katika muda wa majuma kadhaa yaliyopita.
Trump ananuia kuwarejesha kimabavu mamilioni ya waliohamia nchini humo kiharamu na serikali yake imeimarisha mikakati ya kuwafurusha ikiwemo kuwatuma wahalifu waliohukumiwa baada ya kupatikana na hatia katika mataifa mawili ya Afrika, Sudan Kusini na Eswatini.
Wahamiaji wanaopatikana na hatia kwa kawaida hutumikia vifungo vyao kwanza nchini humo kabla ya kurudishwa makwao.
Hii ni sawa na kisa ambapo wanaume wanane walirudishwa Sudan Kusini na watano Eswatini, japo baadhi yao walikuwa wameachiliwa awali.
Wizara ya Usalama wa Ndani (DHS) nchini humo ilisema Juni kwamba mchakato wa kuwapeleka katika mataifa maskini huwaruhusu kuwarejesha watu “katili kupindukia kiasi kwamba nchi zao zenyewe haziwezi kuwakubali kurejea”.
Wakosoaji wamepinga vikali uamuzi huo wakisema kuwa haijathibitishwa ikiwa Amerika ilijaribu kuwarejesha wanaume waliorushwa Sudan Kusini na Eswatini katika mataifa yao na kwamba mchakato wa kuwarejesha ulikuwa wa kinyama.
Reuters ilibaini wanaume wasiopungua watano waliotishiwa kusafirishwa kimabavu Libya mnamo Mei, walirejeshwa mataifa yao wiki kadhaa baadaye, kulingana na mahojiano yaliyoshirikisha wanaume wawili, jamaa na mawakili wa familia.
Baada ya jaji wa Amerika kuzuia serikali ya Trump kuwarusha Libya, wanaume hao wote; wawili kutoka Vietnam, wawili kutoka Laos na mmoja wa Mexico, walirejeshwa makwao nchini mwao.
Hatua ya kuwarejesha haijaripotiwa hapo mbeleni.
DHS haikuzungumzia utimuaji huo.
Reuters haingeweza kubainisha iwapo nchi zao zilikuwa zimekataa awali kuwapokea au sababu ya Amerika kujaribu kuwarusha Libya.
Msemaji wa DHS, Tricia McLaughlin, alipinga kuwa nchi za majambazi waliorushwa mataifa maskini zilikuwa tayari kuwapokea, lakini hakueleza kwa kina kuhusu juhudi zozote za kuwarejesha wanaume hao watano makwao kabla ya wao kutishiwa kutupwa Libya.
“Ukija taifa letu na kuvunja sheria zetu, huenda ukaishia CECOT, Alligator Alcatraz, Guantanamo Bay, au Sudan Kusini au taifa lingine maskini,” alisema McLaughlin kupitia taarifa akirejelea gereza kuu la El Savador na jela iliyopo Florida Everglades.
DHS haikujibu chochote kuhusu idadi ya waliorushwa katika nchi maskini tangu Trump alipochukua usukani Januari 20, japo kuna maelfu waliorejeshwa Mexico na mamia katika nchi nyinginezo.
Wanaume wanane waliorushwa Sudan Kusini wanatoka Cuba, Laos, Mexico, Myanmar, Sudan Kusini na Vietnam, kulingana na DHS.
Mwanamme ambaye DHS ilisema anatoka Sudan Kusini alikuwa na amri ya kumrudisha kutoka Sudan, kulingana na kesi iliyowasilishwa kortini.
Wanaume watano waliorushwa Eswatini wanatoka Cuba, Jamaica, Laos, Vietnam na Yemen, kwa mujibu wa DHS.