Harambee Stars matajiri wapya mjini baada ya kupokea Sh42 milioni za Ruto
UTAJIRI mwishowe ulifika mlangoni mwa wachezaji 27 wa Harambee Stars na maafisa 15 wa benchi ya kiufundi Jumatatu baada ya serikali kuwalipa Sh42 milioni kutokana na ushindi dhidi ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Jumapili.
Kenya ilipiga DR Congo 1-0 katika uga wa MISC Kasarani kwenye mechi ya Kundi A ya kuwania ubingwa wa Kombe la Afrika kwa Wachezaji wanaoshiriki Ligi za Nyumbani (CHAN 2024).
Mchuano huo ulihudhuriwa na viongozi wa serikali akiwemo Rais William Ruto pamoja na Kiongozi wa ODM Raila Odinga.
Wizara ya Michezo pamoja na Msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed jana zilithibitisha kuwa pesa hizo zimelipwa.
Rais William Ruto alikuwa ametoa ahadi ya kila mchezaji na mwanachama wa benchi ya kiufundi wa Harambee Stars walipwe Sh1 milioni kwa kila mechi ambayo watashinda katika kipute hicho kinachoandaliwa Kenya, Uganda na Tanzania.
“Rais William Ruto ametimiza ahadi yake ya kuwalipa Sh1 milioni kila moja kwa wachezaji wote 27 wa Harambee Stars na wanachama 15 wa benchi ya kiufundi, jumla ya Sh42 milioni zimelipwa kufuatia ushindi wa 1-0 dhidi ya DRC mnamo Jumapili,” akaandika Mohamed kwenye ukurasa wake wa X.
“Wizara ya Michezo imetuma pesa hizo na tunu kama hiyo inawasubiri iwapo watashinda Angola mnamo Alhamisi,” akaongeza.
Taifa Leo kivyake ilibaini kutoka kwa Rais wa Shirikisho la Soka Nchini (FKF) Hussein Mohamed kuwa wamelipwa.
“Nakuthibitishia kama mkuu wa FKF kuwa wamelipwa asilimia 100 na unaweza kuninukuu kuhusu hili. Serikali imetimiza ahadi na mimi ni shahidi,” akasema Hussein kwenye mahojiano na Taifa Leo.
Wachezaji wawili pia walithibitishia Taifa Leo kuwa wamepokea pesa hizo na kuondoa shaka kabisa kuwa Rais Ruto alikuwa amewapa ahadi hewa.
“Ni ukweli kwamba ahadi imetimizwa na sasa tuna mori ya kushinda Angola ili tuendelee kutajirika. Tutajituma sana tusiangushe nchi na wakati huo huo tupate pesa,” mmoja wao akasema lakini akaomba asinukuliwe.