Aliyeua babake wakizozania mboga ya sukumawiki auawa na umati
WAKAZI wa kijiji cha Emulwala, Khwisero, Kaunti ya Kakamega wanaomboleza baada ya tukio la kusikitisha ambapo mwanamume mwenye umri wa miaka 39 alimuua babake kwa kisu baada ya kugombana kuhusu mboga ya sukuma wiki, na baadaye akauawa na umati.
Lincoln Topi, mwenye umri wa miaka 39, alimuua babake, Milton Abednego, mwenye umri wa miaka 70, kwa kumkatakata kichwani, kabla ya kushambuliwa na umati wa wakazi waliomvamia Jumatano jioni na kumuua papo hapo.
Mashahidi walieleza kuwa Topi alipatikana katika shamba la babake akiiba sukuma wiki, na alipokabiliwa na babake kuhusu wizi huo, alikasirika na kumvamia.
Alimvamia babake na kumnyang’anya panga kabla ya kumkata kichwani mara kadhaa akamuua papo hapo.
Baada ya tukio hilo, Topi alijaribu kutoroka lakini alinaswa na wakazi waliomshambulia na kumuua kwa kumpiga hadi kufa.
Majirani walimlaumu Topi kwa kuzoea kuiba mboga kutoka kwa shamba la babake na kuzibadilisha na pombe haramu na dawa za kulevya kama bangi.
Kamanda wa polisi wa eneo la Khwisero, Bw Ezekiel Chepkwony, alilaani tukio hilo na kuwataka wakazi kutumia njia za amani kusuluhisha tofauti zao.
Alisema polisi wameanzisha msako mkali dhidi ya pombe haramu na dawa za kulevya zinazozidi kuenea katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa Chepkwony, dawa nyingi za kulevya zinazotumiwa katika eneo hilo huingizwa kutoka miji jirani ya Luanda na Emuhaya katika Kaunti ya Vihiga.
“Eneo letu linapakana na Kaunti ya Vihiga ambako bangi imeenea sana. Wauzaji haramu kutoka maeneo hayo wanashirikiana na wafanyabiashara waovu hapa Khwisero kueneza biashara na matumizi ya dawa hizi haramu,” alisema Bw Chepkwony.
TAFSIRI: BENSON MATHEKA