‘Kazi ya Utumwa’: TSC yapondwa kwa kutaka kuajiri walimu 24,000 kama vibarua
TANGAZO la Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) kuhusu ajira ya walimu vibarua 24,000 limezua upya malalamishi kutoka kwa vyama vya walimu, ambavyo vinashutumu tume hiyo kwa kuwaajiri walimu kwa masharti duni.
Vyama vya walimu vinasema kuwa TSC imeshindwa kutimiza matakwa yao ya muda mrefu, yakiwemo kuajiri walimu vibarua kwa kazi ya kudumu na pensheni, kuongeza viwango vya mishahara, na kushughulikia uhaba mkubwa wa walimu shuleni.
Wanadai kwamba nafasi hizo mpya zilizotangazwa ni kuendeleza sera inayowafunga walimu waliobobea katika ajira za muda zisizo na usalama wala heshima ya kikazi.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu wa Sekondari na Vyuo vya Kadri (KUPPET), Bw Moses Nthurima, ameishutumu serikali kwa hatua aliyoitaja kama “kuwatumia vibaya walimu wanaotafuta ajira badala ya kuwapa kazi za kudumu”.
“Ni jambo la kusikitisha sana serikali inapochukua hatua ya kuwaweka walimu waliobobea, walio tayari kuhudumu, katika hali ya utumwa na mateso, kwa sababu tu inataka kupata nguvu kazi ya bei nafuu. Ikiwa wameunda mfumo ambapo njia pekee ya kuajiri ni kupitia vibarua, na hali hiyo inawaweka watu kwenye umasikini na kukata tamaa, basi ijulikane wazi kuwa tutapinga mfumo huo. Suluhisho pekee kwa uhaba wa walimu ni kuwaajiri kwa masharti ya kudumu na pensheni,” alisema Bw Nthurima.
Vyama hivyo vinaendelea kushinikiza serikali kuacha sera ya kuajiri walimu kwa muda kama suluhisho la kudumu, na badala yake kuwe na mpango wa wazi wa kuajiri walimu wote waliopata mafunzo kikamilifu kwa masharti ya kudumu.
Alieleza kuwa hakuna sheria inayoruhusu TSC kuwaajiri walimu kwa masharti ya muda kama walimu wanagenzi (internship), na kuongeza kuwa malalamiko ya awali kutoka kwa vyama vya walimu hayajashughulikiwa.
“Tulipendekeza kuwa walimu wanaoajiriwa vibarua walipwe angalau Sh25,000 kwa mwezi, sawa na wanavyolipwa wahitimu wengine serikalini. Badala ya kurekebisha hali hiyo, serikali imeamua kuendelea kuwalipa walimu Sh17,000, jambo ambalo halikubaliki,” alisema.
Bw Nthurima alifichua kuwa taifa linakabiliwa na upungufu wa walimu wapatao 116,000, lakini badala ya kuajiri wa kudumu, serikali imeamua kutumia mfumo wa ajira ya muda kwa malipo duni.
“Hii ni sera iliyobuniwa na serikali ili kuonyesha kana kwamba walimu wanaajiriwa ilhali ukweli ni kwamba wanawatumia bila kuwapa haki zao. Mpango huu umetumiwa kwa faida ya kisiasa,” aliongeza.
KUPPET na vyama vingine vya walimu sasa vinashinikiza serikali kusitisha mpango wa ajira ya muda na kuanzisha mfumo wa wazi wa kuwaajiri walimu wote waliohitimu kwa masharti ya kudumu na marupurupu yanayostahili.