Lugha, Fasihi na Elimu

Matumizi yasiyofaa ya kiambishi {ki} katika vichwa vya habari (Sehemu ya 2)

Na ENOCK NYARIKI August 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

TULITAMATISHA sehemu ya kwanza ya makala kwa kueleza kuwa kichwa cha habari tulichokinukuu katika utangulizi wa makala hayo kunaibua utata.

Kimsingi, kichwa chochote cha habari hukusudiwa kunasa macho ya msomaji huku kwa njia ya muhtasari kikiwasilisha ukweli katika matini.

Hata hivyo, matumizi ya kiambishi {ki} katika “Wasiwasi magaidi wakilenga kambi za polisi wa GSU Lamu” yanaibua utata wa kiwakati.

Ijapokuwa mwandishi wa kichwa hiki cha habari alikusudia kuonyesha jinsi uvamizi wa kambi za polisi wa GSU ulivyozua wasiwasi, matumizi ya kiambishi {ki} kueleza hali hiyo yanaishia kuupotosha ujumbe.

Kiambishi {ki} kilivyotumiwa katika kichwa hicho kinazua dhana ya masharti. Kinaonyesha hali inayotarajiwa endapo magaidi watavamia kambi za polisi wa GSU.

Kwa njia nyingine, kiambishi hicho kinaashiria wakati ujao. Hali hii inakinzana na dhana ya ‘upya’ (immediacy) wa taarifa za habari.

Kwa muhtasari, kichwa cha habari tunachokijadili katika makala haya kimeandikwa kivoloya. Inawezekana kukiandika upya kwa kuzingatia iktisadi huku dhana ya ‘upya’ (immediacy) wa habari ikidumishwa.

Tutafanya hivyo kwa kutumia hali isiyodhihirika ya wakati uliopo. Tazama mfano huu: Magaidi walenga kambi za polisi wa GSU na kuzua wasiwasi.

Kichwa hiki cha habari kimewasilisha ujumbe uliokusudiwa kwa kutumia iktisadi ya maneno na kwa kuzingatia kipengele cha ‘upya’ (immediacy) ambacho ni muhimu sana katika taarifa za habari.

Makala yajayo yatajadili matumizi mwafaka ya kiambishi {ki} cha hali.

…YATAENDELEA

enyarikinyariki@gmail.com