Gen Z afanikiwa kuondolewa risasi ya polisi mwilini baada ya siku 400
MATUMANI ya kuanza maisha upya kwa Samuel Kinyajui, 30, kutoka Roysambu, Nairobi yamerejea baada ya hospitali ya Ladnan kukamilisha zoezi la upasuaji na kutoa risasi aliyoishi nayo kwa zaidi ya siku 400.
Kinyajui alipigwa risasi wakati wa maandamano ya Gen Z ya mwaka 2024 na kukimbizwa katika hospitali Kuu ya Kitaifa ya Kenyatta kwa matibabu.
Alifanyiwa upasuaji wa Julai 16, 2024 na kuruhusiwa kwenda nyumbani Septemba 18 mwaka huo.
Hata hivyo, kabla ya kuondoka katika hospitali hiyo, daktari aliyehusika na upasuaji wa kwanza alimweleza kuwa kipande cha risasi kilichosalia anaweza kuishi nacho.
“Baada ya upasuaji, daktari alinionyesha picha ya risasi iliyoondolewa na kunihakikishia kuwa kipande kilichosalia naweza kuishi nacho kwenye mwili wangu. Lakini haijakuwa rahisi, nimekuwa nikihisi uchungu wa mara kwa mara na kunilazimisha nitumie tembe kumi za kupunguza uchungu huo,” alisema Kinyajui.
Mateso hayo yalichangia kutafuta matibabu katika hospitali ya Ladnan mwaka huu. Hospitali hiyo, ilithibitisha kuwa risasi hiyo inaweza kutolewa na maisha yake kurejea kama kawaida.

Agosti 13, 2025, Kinyajui alijihami na stakabadhi kutoka kwa Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi (IPOA) kama jinsi alivyokuwa ameagizwa na daktari wake ili kuwezesha kuondoa risasi mwilini mwake.
Saa kadhaa baadaye, alirejeshwa kwenye chumba ya kutuliza maumivu akiwa na tasabamu tele baada ya upasuaji kukamilika na risasi kuondolewa.
“Nina furaha baada ya risasi kutolewa mwilini mwangu. Upasuaji huo ulikuwa rahisi mno, daktari alitumia dakika 20 pekee. Kwa sasa nina matumaini ya kuona,” alisema Kinyajui baada ya upasuaji.
Rafikiye, Njiiri Gatauri ambaye amekuwa akimpa makao, ametaka serikali kuwajibikia malalamishi ya Vijana wa Gen Z akisema kuwa hayafai kupuuzwa kamwe.
“Ameishi na uchungu huo kwa zaidi ya siku 500. Hii ni risasi na chuma tuu. Alama aliyosalia nayo ni kutokana na malalamishi ambayo Gen Z wanataka serikali ishughulikie. Nina furaha sana leo risasi imeondolewa kwenye mwili wake,” alisema Bw Gatauri.
Wakati huo uo, Bw Kinyajui alisikitishwa na madai ya daktari wa kwanza katika hospitali kuu ya Kitaifa ya Kenyatta ambaye alimweleza kuwa, anaweza kuishi na kipande hicho.
“Kwa uhakika nilidanganywa, Kenyatta waliniruhusu kuondoka na risasi. Leo nimeona ikiwa zima sio kipande jinsi niliambiwa,” alisisitiza Bw Kinyajui.

Risasi hiyo ilichukuliwa na maafisa wa IPOA ambao walifika kutathimini hali ilivyokuwa. Hali ambayo kijana huyo ana matumaini ya kupata haki.
“Nina imani IPOA itanitafutia haki. Naamini IPOA itanipa haki yangu na afisa aliyehusika atachukuliwa hatua kali.”
Mwanaharakati kutoka Shirika la Vocal Afrika Bw Odhiambo Ojiro, ambaye alifika kushuhudia upasuaji huo, aliitaka serikali kuomba msamaha kutokana na mauaji ya vijana wa Gen Z.
“Kile tunataka kutoka kwa serikali ni iombe msamaha kwa umma kwa kutekeleza mauaji ya vijana wa Gen Z. Tunataka wahusika wachukuliwe hatua kwa kuwaua vijana wadogo. Tunataka maafisa hao, wakamatwe na kufunguliwa mashtaka kabla ya kuazisha mchakato wa jinsi waathiriwa wanafaa kulipwa,” alisema Bw Ojiro.