Ukraine roho mkononi ikiombea Trump asiwapige bei kwa Putin
ALASKA, AMERIKA
HUKU Kongamano la Amerika-Urusi likiandaliwa leo, Rais Volodymyr Zelenskiy Alhamisi alitembelea London kuhakikisha kuwa Ulaya inaunga mkono makubaliano yoyote ambayo yatahakikisha ardhi ya Ukraine haiingiliwi.
Kongamano la Ijumaa ambalo litaongozwa na Rais Donald Trump na Vladimir Putin wa Urusi, ni mtihani mkubwa kwa Ukraine tangu vita kati yao na Urusi vianze.
Vita hivyo, vilivyoanza mnamo Februari 2022 vimechangia mauaji mengi huku mamilioni wengine wakilazimika kuhama makwao.
Zeleskiy na wandani wake Ulaya wanamakinika kuhakikisha kuwa mkataba wowote kati ya Amerika na Urusi ambao utawaacha Ukraine kuwa dhaifu mkononi mwa adui wake haufikiwi.
Zelenskiy Alhamisi alikutana na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer kuangazia tena yaliyofikiwa wakati wa mkutano ulioandaliwa mnamo Jumatano ambapo mataifa ya EU yalikubali kusimama na Ukraine.
Pia mataifa hayo yaliafikiana kuhusu masuala ambayo kongamano la Amerika-Urusi halifai kugusia kuhusu Ukraine.
Mnamo Jumatano, Trump alitishia kuangushia Urusi adhabu kali iwapo Putin hatakubali kulegeza kamba na kumaliza vita dhidi ya Ukraine.
Mara si moja ameweka wazi kuwa Amerika iko tayari kuangushia Urusi adhabu kali iwapo haitaridhiana na Ukraine na kusitisha vita.
“Mkutano na mataifa ya EU yaliyosisitiza haja ya amani, ulifana kabisa na tunataraji kuwa amani itapatikana ili kuwe na usalama na udhabiti wa taifa letu,” akaandika Waziri wa Masuala ya Nje wa Ukraine Andrii Sybiha.
Urusi imekuwa ikipinga shinikizo za EU na Ukraine huku Putin akisisitiza kuwa msimamo wake wa miaka mingi kuhusu vita dhidi ya Ukraine haujabadilika.
Urusi inadhibiti asilimia tano ya ardhi za Ukraine na Trump amekuwa akipendekeza nchi hizo zikubaliane na kubadilishana ardhi.
Ukraine hata hivyo imekuwa ikifasiri hilo kama kuruhusu Urusi iingilie ardhi yake zaidi.