EACC yaandama Nick Mwendwa, Katibu wa zamani warudishe Sh220.4 milioni
TUME ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imewasilisha kesi mahakamani ikitaka kurejesha Sh220.4 milioni kutoka kwa maafisa watano wa zamani, akiwemo Katibu wa zamani wa Wizara ya Michezo chini ya utawala wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, Bw Peter Kaberia, na aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka Kenya (FKF), Bw Nick Mwendwa, kwa madai ya ukiukaji wa sheria za ununuzi wakati wa maandalizi ya mashindano ya CHAN 2018 ambayo hayakufanyika nchini.
Kesi hiyo imewasilishwa baada ya serikali kuondoa kesi ya jinai iliyokuwa ikiendelea kuhusu sakata hiyo.
Wengine waliotajwa katika kesi hiyo ni John Ruga (mhandisi Sports Kenya), Haron Komen (Mkurugenzi wa Utawala katika Wizara ya Michezo), Isaac Okoth, na mkandarasi kutoka Ufaransa, Gregori International.
Kesi inahusu malipo yaliyofanywa kwa kampuni ya Ufaransa mwaka 2017 kuboresha viwanja vya michezo kujiandaa na mashindano ya CHAN 2018 ambayo hatimaye yalihamishiwa Morocco baada ya Kenya kushindwa kutimiza masharti yaliyohitajika.
Kwa mujibu wa EACC, pesa hizo zililipwa kinyume na sheria za ununuzi na mkataba wake ulikuwa na dosari za rushwa na udanganyifu.
kwa ajili ya mashindano hayo, ikiwa ni pamoja na kuchora, kuandaa ardhi, kupanda nyasi maalum (Bermuda/Pasalum), na kuweka vifaa vya michezo.
Mahakama Kuu imezuia kwa muda Wizara ya Michezo kufanya malipo yoyote zaidi kwa kampuni ya Gregori International hadi kesi itakapotatuliwa. Washitakiwa wanatarajiwa kujibu mashtaka hayo rasmi mahakamani.
EACC inadai kuwa sheria mbalimbali zilikiukwa, zikiwemo Sheria ya Kupambana na Ufisadi na Uhalifu wa Kiuchumi, Sheria ya Ununuzi wa Umma, na Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma.
Tume hiyo inadai kuwa malipo yaliyofanywa kwa kampuni hiyo hayakuwa na nyaraka halali za kuthibitisha kazi zilizofanyika.
Pia, inasema kuwa mkataba huo ulisainiwa Septemba 14 2017, ilhali kampuni hiyo ilisajiliwa rasmi nchini Oktoba 31 2017 takriban mwezi mmoja baada ya mkataba kusainiwa.
EACC pia inataka mahakama itangaze kuwa mchakato wa utoaji wa mkataba huo kwa kampuni ya kigeni haukuwa wa kikatiba na ulikiuka sheria za nchi.