KIRIGITI, KIAMBU
TANIBOI wa hapa ameunda kikundi cha marafiki cha kumfanyia mchango ili kugharamia hasara aliyosababisha akijifunza kuendesha gari.
Kijana alikuwa ameletwa na mjomba wake ambaye husafirisha mizigo katika mtaani huu, ili awe taniboi kwa gari lake hilo.
Gari hilo huwa linaegeshwa karibu na vibanda vya chakula kwani ndipo kazi za kusafirisha bidhaa huwa nyingi ikiwemo mizigo ya akina mama mboga.
Siku ya kioja hakukuwa na kazi nyingi hivyo mwenye gari akapata nafasi kwenda jijini kutafuta vipuri kwani kulikuwa na vifaa kadha vya gari vilivyohitaji kurekebishwa.
Mjomba akamuachia ufunguo kwa sharti kwamba kazi ikitokea ampe mmoja wa madereva wanaofanya kazi nao.
Kumbe ingekuwa kisa cha paka akiondoka, panya hutawala. Mjomba alipopiga kona taniboi alichukua ufunguo na kungurumisha gari kwa nia ya kuliendesha.
Hata hivyo, badala ya kuweka gia ya kwenda mbele gari lilienda nyuma na kugonga jiko la supu ya vichwa na mitura ikamwagika na kuleta hasara kubwa.
Mwenye jiko alitoka ndani ya kibanda akiwa amechemka hataki pole zozote. Aliapa kwamba iwapo hatalipwa kila kitu kilichoharibika angewaita polisi wamkamate kijana huyo kwa kuendesha gari bila leseni.