Diamond League: Macho kwa mwanadada Lemngole, mfalme wa 800 Wanyonyi
DORIS Lemngole ana fursa nzuri ya kuonja ushindi wake wa kwanza kabisa kwenye riadha za Diamond League atakapotimka katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji mjini Lausanne, Uswisi, Jumatano.
Macho pia yatakuwa kwa bingwa wa Olimpiki wa 800m Emmanuel Wanyonyi atakayepimwa vilivyo na wakimbiaji kama bingwa wa dunia Marco Arop kutoka Canada, Waamerika Bryce Hoppel na Josh Hoey, Mhispania Mohamed Attaoui, Muingereza Max Burgin na Tshepiso Masalela kutoka Botswana, miongoni mwa wengine.

Wanyonyi anaorodheshwa nambari moja duniani katika 800m. Anajivunia muda bora katika mizunguko hiyo miwili wa dakika 1:41.11 ambao alipata mjini Lausanne mwaka jana.
Wanyonyi,21, ambaye alitawala duru za Oslo (Norway), Stockholm (Uswidi), Monaco (Monaco) na London (Uingereza), amekuwa akijaribu kuvizia rekodi ya dunia ya Mkenya mwenzake David Rudisha ya 1:40.91 ambayo imekuwa imara tangu Agosti 9, 2012. Alikosa rekodi hiyo kwa chini ya sekunde (0.1) mwaka jana na huenda ana mipango ya kuivizia tena Jumatano.
Lemngole, ambaye yuko katika timu ya taifa ya Kenya ya Riadha za Dunia 2025, alishiriki Diamond League mara ya kwanza wakati wa duru ya Doha nchini Qatar mwezi Mei 2023. Wakati huo, hakukamilisha 3,000m kuruka viunzi na maji.
Lemngole kukosa upinzani wa wakali Yavi, Cherotich
Mtimkaji huyo mwenye umri wa miaka 23 anayesomea nchini Amerika, aliandikisha muda wa kuridhisha baada ya kukamilisha umbali huo kwa dakika nane na sekunde 58.15 wakati wa mashindano ya vyuo vikuu vya Amerika mjini Eugene mnamo Juni 14, 2025.
Kabla ya hapo, muda wake bora katika 3,000m kuruka viunzi na maji ulikuwa 9:15.24 ambao pia alipata kwenye mashindano hayo ya vyuo mjini Eugene mnamo Juni 8, 2024.
Hapo Jumatano, Lemngole atatoana kijasho na mzawa wa Kenya Norah Jeruto kutoka Kazakhstan (8:59.46), Waethiopia Sembo Almayew (8:59.90), Alemnat Walle (9:06.88), Wosane Asefa (9:20.83), Firehiwot Gesese (9:32.09) na Meseret Yeshaneh (9:47.29), pamoja na washiriki kutoka Amerika, Ujerumani, Poland na Uingereza.
Bingwa wa Olimpiki na dunia Winfred Yavi kutoka Bahrain, ambaye alizaliwa Kenya, mshindi wa nishani ya medali ya shaba ya Olimpiki Faith Cherotich, na bingwa wa zamani wa Olimpiki Peruth Chemutai hawakuingia duru ya Lausanne.

Denis Kipkoech, Ishmael Kipkurui, Jacob Krop na Edwin Kurgat watashiriki 5,000m ambapo watakabiliana na wakali kama Thierry Ndikumwenayo (Uhispania), Hagos Gebrhiwet na Samuel Tefera (Ethiopia), Isaac Kimeli (Ubelgiji), Graham Blanks (Amerika), Balew Birhanu (Bahrain) na Filip Ingebrigtsen (Norway). Itakuwa fursa nzuri ya Wakenya kuwinda tiketi ya kuingia Riadha za Dunia zitakazofanyika mjini Tokyo, Japan.