Buchari dijitali kuuza nyama jijini
JANGA la Covid-19 lilipotua nchini 2020, shughuli nyingi za kibiashara zilisambaratika, na Martin King’ori, ambaye ni mfanyabiashara katika sekta ya nyama hakusazwa.
Wajasiriamali hasa walioko Nairobi, viunga vyake na kaunti jirani walilemewa na amri ya ama kuingia au kutoka jijini kufuatia marufuku ya kusafiri na vizuizi vilivyowekwa ili kusaidia kudhibiti msambao zaidi wa virusi vya ugonjwa huo wa kimataifa, corona.
Aida, biashara nyingi zilisitisha shughuli zake kwa muda.
Ingawa sekta ya chakula iliendeleza huduma zake, King’ori alilazimika kuwa mbunifu ili kuendelea kuhudumia wateja wake kwa bidhaa za nyama.
Akiwa amebobea katika masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT), alitumia maarifa yake ya kidijitali kuziba pengo hilo na kuhakikisha wateja wake hawakukosa kitoweo walichozoea.

“Covid ilitokea wakati biashara yangu ilikuwa imeanza kushika kasi. Katika ujasiriamali na biashara, lazima uwe mbunifu na mwepesi wa kufikiri nje ya boksi. Teknolojia ni nguzo muhimu mno kwenye maendeleo,” anasema King’ori.
Akiwa na Diploma ya IT, alitumia maarifa yake kuunda jukwaa la kidijitali kuhudumia wateja kwa urahisi, hasa kipindi ambacho walimhitaji zaidi.
Wazo hilo lilizaliwa kutokana na wingi wa oda kupitia simu majira ya jioni alizopokea, lakini marufuku ya kusafiri ilizuia wanunuzi wa nyama kumfikia.
“Niliamua kuunda apu ya kidijitali, ambayo imewafaa wateja wangu kwa kiwango kikubwa,” anasema.
Apu hiyo, iliyoanza kama jaribio, ilizinduliwa rasmi kwenye mtandao wa Google Play Store mwaka wa 2022 na sasa inapatikana kwa yeyote mwenye simu ya Android.

Kwa kuanzia na duka moja la buchari, King’ori ameweza kupanua biashara hadi kuwa na jumla ya matawi manne.
Buchari yake ya kwanza ipo Kasarani, Nairobi, na aliianza na mtaji wa Sh300,000 aliopata kutokana na kazi za ICT.
Chini ya nembo Camp David Butchery, sasa anaendesha buchari mbili Kasarani eneo la Clayworks, nyingine Mirema–Zimmerman, na moja Githiga, Githunguri, Kaunti ya Kiambu, ambako pia ana kituo cha kulisha mifugo ili kuwanenepesha (feedlot) anapowanunua kutoka kwa wafugaji.
Aidha, kituo hicho kina uwezo wa kuhifadhi wanyama 30, wanaotoka kwa wafugaji zaidi ya 1,000 kutoka kaunti ya Kajiado, Narok na Laikipia – ambazo zinaorodheshwa kama maeneo kame na nusu kame (ASAL).
“Ili kuafikia ubora wa nyama, nilianzisha feedlot kunenepesha ng’ombe kwa miezi miwili au mitatu. Wanapewa lishe bora yenye madini na virutubisho,” King’ori akaambia Akilimali kwenye mahojiano ya kipekee.

Hatua hiyo inamsaidia kuhakikisha nyama zinazotua kwenye sahani ni salama.
Hali kadhalika, King’ori ana ranchi eneo la Suswa, Narok, yenye zaidi ya ng’ombe 40.
Uamuzi wake kuwekeza kwenye huduma kwa njia ya kidijitali unaambatana na matakwa ya Mswada wa Kudhibiti Usalama wa Chakula na Malisho wa 2023 uliopo kwenye steji ya mwisho kupitishwa kuwa sheria.
Nyama anazouza ni pamoja na T-bone, ribeye, sirloin, brisket, chuck, osso buco, na nyinginezo.
Pia, ana bidhaa zilizoongezwa thamani kama vile dry-aged beef, soseji, mutura, burgers, na samosa.
Asilimia 40 ya wateja wake huagiza bidhaa mtandaoni – kupitia apu ya Camp David aliyozindua.
Bei huanzia Sh700 hadi Sh1,800 kwa kilo kulingana na aina ya nyama.

“Tunatumia mitandao kama TikTok, Instagram, Facebook, X (awali Twitter), na apu yetu. Mteja akijisajili, anaweza kuona bidhaa zote na kuagiza anayotaka,” anaelezea.
Apu ya Camp David imeunganishwa na M-Pesa, huku kila oda ikiwa na msimbo, yaani code, wa kipekee kwa usalama kuhakikisha anayeagiza nyama ndiye mteja halisi.
“Tuna wahudumu wa bodaboda ambao husambaza bidhaa, na kabla kupeana kwa mteja sharti aonyeshe msimbo aliopokea.”
Wanabodaboda hao wamepigwa msasa kwa stakabadhi rasmi; kupeana nakala zao za umiliki wa pikipiki, leseni, kitambulisho na picha, kuhakikisha uadilifu na usalama wa bidhaa.
Nyama, King’ori amekumbatia mfumo maalum kuhakikisha hazichakachuliwi – vacuum packaging.

Alianza na wafanyakazi wawili, na sasa ameajiri watu 15 kwa njia ya moja kwa moja, na wengine 25 kwa njia isiyo ya moja kwa moja.
Hata hivyo, anakiri idadi ya wateja imeshuka akilinganisha na mwaka wa 2020, kibarua kikiwa kupata hela zaidi hasa mikopo kutoka kwa mashirika ya kifedha kupanua huduma zake.
Huhudhuria Maonyesho ya Nyama ya Kenya (Kenya Meat Expo & Conference) yanayoandaliwa na Nation Media Group (NMG) PLC, akisema yamemsaidia kuuza bidhaa zake kama vile dry-aged beef.
Makala ya Nne ya maonyesho hayo yatafanyika katika ukumbi wa KICC, Nairobi, kuanzia Agosti 6 hadi 8, yakileta pamoja wadauhusika wa sekta ya nyama na mifugo na kutoa jukwaa kwa wakulima kujifunza mengi kuhusu ufugaji.