• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 1:29 PM
Nyama ya kasa ni marufuku nchini licha ya walaji kudai inaepusha pumu

Nyama ya kasa ni marufuku nchini licha ya walaji kudai inaepusha pumu

NA KALUME KAZUNGU

LICHA ya kwamba sifa za nyama ya kasa zimeenea kote Pwani ya Afrika Mashariki kwamba inasaidia mlaji kukabiliana na maradhi ya pumu na kuimarisha umachachari chumbani, ni marufuku kumvua kasa nchini Kenya.

Baadhi ya wakazi kwenye visiwa mbalimbali vya Lamu wanasema minofu ya kasa ni tamu kushinda nyama nyingine yoyote ile.

Kasa ni mnyama wa baharini afananaye na kobe na ambaye huwa na magubiti makubwa.

Mnyama huyo huzaa kupitia mayai, ambapo huyataga kwenye nchi kavu, hasa katika fukwe zilizojificha za Bahari Hindi na ambazo zina mchanga mwingi.

Licha ya serikali ya Kenya mnamo 2002 kuweka au kutangaza sheria inayopiga marufuku matumizi ya kasa, mayai, nyama, mafuta au magamba yake, bado kumekuwa kukirekodiwa visa vya watu kumwinda mnyama huyo kisiri, kumchinja na kula nyama yake.

Kuna matukio ambapo watu wamekuwa wakisakwa na kukamatwa na maafisa wa Shirika la Huduma kwa Wanyamapori nchini (KWS) kwa kupatikana wakiwa wamemvua na kummiliki kasa au viungo vyake.

Mnamo Septemba 2016, mwanamume kwa jina Bwasadi Lali,45, alikamatwa na maafisa wa KWS akiwa na karibu kilo 50 za nyama ya kasa kisiwani Pate, Lamu Mashariki.

Lakini je, umewahi kujiuliza mbona kula nyama ya kasa?

Wenyeji wa mwambao wa Pwani, hasa wale wa visiwa mbalimbali vya Lamu, wanaitaja nyama ya kasa kuwa na manufaa tele kwa binadamu.

Bw Harun Athman, mkazi wa kisiwa cha Lamu, anasema mbali na utamu wake, nyama ya kasa na mafuta yake ni kinga na tiba tosha kwa wanaougua maradhi ya pumu.

Pumu ni ugonjwa wa mapafu unaomfanya mgonjwa awe na shida ya kupumua.

Bw Athman anasema yeye binafsi amekua huku akiona au kushuhudia vile mababu na wazee pale mtaani kwao walikuwa wakichangamkia nyama au mafuta ya kasa kuwatibu waliokuwa wakiugua pumu.

“Mbali na pumu, nyama ya kasa husaidia kukabiliana na maradhi mengine yoyote yanayohusiana na mapafu au matatizo yoyote yale ya kupumua kama kifua kikuu (TB). Kwa wanaougua pumu au TB punde wakila nyama ya kasa na kunywa supu na mafuta ya kasa, wanapata afueni,” akasema Bw Athman.

Mzee Mohamed Mbwana, anasema ndoa nyingi zilizokuwa katika hatari ya kusambaratika Lamu na Pwani kwa ujumla kutokana na wanaume kukosa hamu ya kustarehe na wake zao, zinapona kupitia ulaji wa nyama ya kasa na mafuta yake.

Kulingana na Bw Mbwana, nyama au mafuta ya kasa ni zaidi ya tembe za viagra almaarufu ‘blue pills’ kwani wanaume wengi wanaokosa nguvu za kiume wamejipata wakifanya vyema kwa wake au wapenzi wao kitandani punde wanapoila.

“Tofauti na viagra ambayo huleta athari ya mtu kupandwa na presha au shinikizo la damu na moyo, nyama ya kasa, supu na mafuta yake havina madhara. Ni tiba asili ya nguvu za kiume licha ya kwamba serikali inaonya raia kumvua mnyama huyo,” akasema Bw Mbwana.

Mnamo 2019, wakazi wa visiwa mbalimbali vya Lamu, ikiwemo Pate, Kiwayu, Ishakani, Shanga, Rubu, Mkokoni, Kizingitini, Mtangawanda, Faza na viunga vyake waligonga vichwa vya habari pale walipoirai serikali kuifanyia marekebisho au kuondoa kabisa sheria inayopiga marufuku uvuaji na ulaji wa kasa kwa madai kuwa imechangia ndoa nyingi kusambaratika eneo hilo.

Wakazi hao, wengi wao wakiwa ni wavuvi, walilalamika kuwa nguvu zao za kiume zimepungua pakubwa, hasa tangu walipoanza kukosa madini muhimu kutoka kwa nyama, mafuta au supu ya kasa ambaye serikali hairuhusu avuliwe, auawe au kuliwa.

Wavuvi hao walishikilia kuwa talaka nyingi maeneo yao zilikuwa zikichangiwa na kupungua kwa nguvu za kiume miongoni mwao kunakochangiwa na kukosa kula kasa.

Soma Pia: Jinsi nyama ya kasa inavyotayarishwa kuepuka vifo kama vilivyotokea Zanzibar

Waliisisitizia serikali kuwaruhusu wavue kasa ili wapate kufaidi nyama na mafuta yake.

“Sheria iliyopo kuhusu kasa na marufuku yake ikarabatiwe. Furaha yetu ni kuona tumeruhusiwa kumvua na kumla huyu kasa bila ya uoga wa kukamatwa,” akasema Bw Kassim Shee, mkazi wa kisiwa cha Kizingitini.

Bw Ali Abdalla aliikashifu serikali kwa kuwakandamiza wakazi kupitia marufuku ya kutomvua kasa.

Bw Abdalla alisema wavuvi Wabajuni wa Lamu ndio nambari moja katika masuala ya uhifadhi wa viumbe wa baharini, ikiwemo kasa na kwamba kuwapiga marufuku ya kumvua na kumtumia mnyama huyo si jambo jema.

“Serikali ijilaumu yenyewe inaposema kasa wako kwenye hatari ya kuangamia. Ifahamike kwamba kasa anahitaji ufukwe wa bahari wenye mchanga mwingi na tulivu ili akague mahali pa siri pa kutagia mayai na kuangua watoto wake. Serikali imeruhusu sehemu hizo za fukwe za bahari kunyakuliwa au kuziwa mabepari. Wamejenga kwenye fukwe hizo, hivyo kumkosesha kasa eneo mwafaka la kuzalia. Warekebishe hilo na waache wananchi kula huyo kasa kwani sisi hatuwezi kumaliza idadi yao. Hatari iliyoko ni unyakuzi wa maeneo ya fukwe ambayo hawa kasa kuyatumia kuzaa,” akasema Bw Abdalla.

Kwa upande wake, Afisa Msimamizi wa KWS Kaunti ya Lamu Ahmed Ibrahim, alishikilia kuwa serikali iko imara na kwamba inaendeleza juhudi za kuhakikisha kasa wachache waliopo nchini kwa sasa wanalindwa vilivyo ili kuepuka kuendelea kuwa katika hatari ya kuangamia.

Bw Ibrahim alisema doria za kila mara zimekuwa zikiendelezwa kwenye Bahari Hindi na fukwe mbalimbali kote Lamu kuona kwamba kasa hawauawi au kuvuliwa baharini.

Alitaja kisa cha hivi majuzi ambapo wanaume watatu walikamatwa wakiwa na kasa hai waliyekuwa wamembeba kwenye mashua yao eneo la Kiunga, mpakani mwa Kenya na Somalia.

“Tuliwashika wavuvi hao na kuwapeleka kortini walikofunguliwa mashtaka. Kesi inaendelea. Isitoshe, tunaendeleza hamasa kwa wananchi, hasa wavuvi waachane kabisa kumlenga na kumuua kasa eti kwa sababu ya kula nyama yake. Watafute samaki wa kawaida ili wale badala ya huyu kasa. Ni mnyama ambaye idadi yake ni ndogo nchini,” akasema Bw Ibrahim.

Afisa huyo aidha aliwashukuru wananchi wa Lamu kwa ushirikiano wao katika kumlinda kasa na viumbe wengine walioko kwenye hatari ya kuangamia.

“Wananchi ninawasihi tuendelee kushirikiana kumlinda kasa na wanyama wengine adimu hapa Lamu, Pwani na Kenya kwa ujumla tukiwa kama timu moja. Wavuvi wengi hapa Lamu ni wangwana,” akasema Bw Ibrahim.

  • Tags

You can share this post!

Baraza la Mawaziri launga vita dhidi ya vileo haramu

Jinsi mzee alivyouawa na gari la mbunge aliyempigia kampeni

T L