Habari

Msichana, 9, aadhibiwa kikatili na wazazi wake kwa kuchelewa kanisani

Na MERCY KOSKEI, JOHN NJOROGE August 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MSICHANA mwenye umri wa miaka tisa kutoka Kijiji cha Chepkinoyo, wadi ya Nyota katika eneo la Kuresoi Kaskazini, Kaunti ya Nakuru, anauguza majeraha mabaya baada ya kushambuliwa kinyama na wazazi wake.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Kuresoi Kaskazini, Bw Judas Gathenge, mwanafunzi huyo wa darasa la tano alishambuliwa mnamo Agosti 17 na mama yake, Bi Tabitha Wanjiku, kwa madai ya kuchelewa kurudi nyumbani kutoka kanisani.

Bw Gathenge alieleza kuwa mama huyo, pamoja na baba wa kambo wa mtoto huyo, Bw Peter Maina, walimvua nguo, wakamfunga mikono na kumshambulia kwa kipigo kikali.

“Tulipomkagua, alionekana kuwa na majeraha ya kuumwa mgongoni pamoja na majeraha mengine mwilini,” alisema Bw Gathenge.

Majirani waligundua tukio hilo Jumatatu na kuvamia nyumba hiyo ambapo walimwokoa mtoto huyo na kumkimbiza hospitalini kwa matibabu.

Mama huyo alikamatwa na kupelekwa katika Kituo cha Polisi cha Temuyota, ambapo anazuiliwa na anatarajiwa kufikishwa mahakamani. Baba wa kambo alitoroka na msako umeanzishwa kumkamata.

Bw Gathenge alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa Bi Wanjiku aliolewa akiwa tayari na mtoto huyo, kabla ya kupata watoto wawili zaidi na mume wa sasa.

Kwa mujibu wa mzee wa kijiji Peter Ngetich, binti huyo alipigwa baada ya kuchelewa kurudi kutoka kanisani, jambo ambalo liliwakera wazazi wake.

“Majirani walivutiwa na kilio kutoka kwa nyumba hiyo. Mwanamke mmoja alipata funguo zilizokuwa karibu na mlango na alipofungua, alikuta mtoto huyo katika hali ya kusikitisha,” alisema.

Aliongeza kuwa msichana huyo alifungiwa ndani ya nyumba siku ya Jumatatu na sehemu ya Jumanne, huku wazazi wake wakiendelea na shughuli zao kana kwamba hakuna kilichotokea.

“Baada ya kumhoji, msichana huyo alieleza kuwa mama yake alikasirika baada ya kukuta vyombo havijaoshwa na kazi nyingine za nyumbani hazijakamilika. Pia alishambuliwa tena usiku alipoingia baba wa kambo,” alisema mzee huyo.

Mtoto huyo alipelekwa katika zahanati ya eneo hilo alikopatiwa dawa za maumivu na kwa sasa anaishi na nyanya yake.