Walimu wenye umri mkubwa kupandishwa vyeo kwanza na mwajiri wao
WALIMU wenye umri wa miaka 57 kwenda juu ambao wamekwama kwenye daraja moja la kazi kwa zaidi ya miaka saba wanatazamiwa kunufaika pakubwa kutokana na nyadhifa 24,000 za kupandishwa vyeo zilizotangazwa mwezi huu.
Mwongozo mpya uliotolewa na Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) umeweka umri wa walimu na muda wanaostahili kudumu kwenye daraja la kazi walimo kwa sasa.
Kulingana na nakala ya alama za mahojiano iliyoonekana na Taifa Leo, mwalimu mwenye umri wa miaka 57 ambaye amedumu kwenye daraja moja la kazi kwa miaka saba, atajinyakulia asilimia 80 ya alama na kuwa kifua mbele kupandishwa cheo moja kwa moja.
Hata hivyo, mwalimu aliye na miaka 41 kwenda chini atapata alama 10 pekee kwenye kitengo cha umri ikilinganishwa na aliye na miaka 57 atakayezoa alama 50.
Mfumo mpya wa alama unagawa alama kwa kuzingatia vipengee kadhaa: kufuzu kielimu na kitaaluma, utendakazi kupitia kipimo cha walimu (TPAD) na majukumu mengineyo kama vile kuhudumu kama watahini, wakufunzi, au wasimamizi wa raslimali.
Walimu wenye viwango vya juu vya kufuzu kielimu na alama za juu za TPAD wanatarajiwa kunufaika zaidi.
“Tume itatumia mwongozo uliopitishwa kwa tathmini ya haki na ufaafu kwa kuzingatia kufuzu kielimu, kuhudumu kama kaimu, muda wa kukaa kwenye daraja, vipimo vya TPAD, ukubwa/tajriba.
Majukumu mengineyo kitaaluma: walimu wanaohusika na KNEC, KICD, MOE, KISE, KEMI, na shughuli za mafunzo ya TSC – TIMEC na CBC watatunukiwa alama maalum kutambua mchango wao,” ilieleza nakala ya alama.
Umri vilevile utachangia wajibu muhimu katika upandishaji vyeo. Mfumo huo unaonekana kuwalemea walimu chipukizi, ambao licha ya stakabadhi thabiti kielimu, watapata alama chache kwenye vitengo vya umri na tajriba.
Kitengo hiki kinatarajiwa kuwafaa walimu waliopevuka kiumri ambao wamekwama daraja moja kwa miaka mingi.