Dimba

Nyota Eberechi Eze kuamua Ijumaa iwapo Arsenal ndio ‘best’

Na MASHIRIKA August 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WINGA wa Crystal Palace, Eberechi Eze ameamua kurejea ‘nyumbani’ Arsenal baada ya kupuuza Tottenham Hotspur waliokuwa wameshamdandia.

Eze, ambaye talanta yake ilipaliliwa na Arsenal kutoka awe na umri wa miaka minane hadi akaachiliwa akiwa na umri wa miaka 13, alikubaliana na Arsenal matakwa ya kibinafsi hapo Jumatano kabla ya shughuli ya kukamilisha uhamisho huo inayotarajiwa leo.

Baada ya kuachiliwa na Arsenal, mchezaji huyo mwenye asili ya Nigeria aliendeleza soka yake katika klabu za Fulham, Reading, Millwal, Queens Park Rangers na Wycombe Wanderers kabla ya kuridhisha zaidi akiwa kambini mwa Palace kiasi cha kuvutia wanabunduki tena.

Spurs walidhani wameshafunga kazi baada ya kufanya mazungumzo na Eze tangu juma lililopita, lakini wamo mbioni kupata aibu kufuatia uamuzi wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 kuchagua Arsenal.

Eze sasa anatarajiwa kufanyiwa uchunguzi wa kiafya leo kabla ya kuhamia ugani Emirates kwa ada ya uhamisho ya Pauni 67.5 milioni.

Arsenal waliamua kujitosa sokoni tena kwa nguvu wiki moja kabla ya kipindi kirefu cha uhamisho kufungwa hapo Septemba 1 baada ya kiungo mshambulizi Kai Havertz kupata jerha la goti.

Eze alitarajiwa kushiriki mchuano wa kufuzu wa dimba la Europa Conference League dhidi ya Fredrikstad jana usiku kabla ya kuambia Palace kwaheri.

Sheria za Shirikisho la Soka la Bara Ulaya (Uefa) linakubalia mchezaji kushiriki mechi za kufuzu kushiriki ligi za Klabu Bingwa Ulaya, Ligi ya Uropa na Conference League kwa hivyo Eze ataweza kuchezea Arsenal katika Klabu Bingwa Ulaya akikamilisha uhamisho.

Dili ya Chelsea kusaini Alejandro Garnacho (Manchester United) na Xavi Simons (Leipzig), Manchester United kuajiri Eduardo Camavinga (Real Madrid) na Lucien Agoume (Sevilla) na kuachilia Rasmus Hojlund pamoja na Manchester City kunyakua kipa Gianluigi Donarumma (PSG), pia zinaaminika kuendelea kuiva.