Makala

Unyakuzi wa ardhi, ufisadi wakithiri kaunti ya Rais Ruto licha ya juhudi nyingi

Na TITUS OMINDE August 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 3

UNYAKUZI wa ardhi umekita mizizi nyumbani wa Rais William Ruto katika Kaunti ya Uasin Gishu licha ya kukerwa kwake na visa vya ufisadi vilivyokithiri bungeni.

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) hivi majuzi iliorodhesha Uasin Gishu miongoni mwa kaunti fisadi zaidi nchini.

Katika ripoti kuhusu ufisadi ya mwaka wa 2024, tume hiyo iliorodhesha Uasin Gishu, Baringo, Embu na Homa Bay kuwa miongoni mwa kaunti fisadi zaidi nchini.

Mnamo Mei 2024, EACC ilitwaa mali ya umma ya thamani ya Sh3.2 bilioni iliyonyakuliwa katika mji wa Eldoret, ikiwa ni pamoja na nyumba ya makazi ya afisa wa mahakama.

Hata hivyo, mwaka mmoja baadaye, hali hiyo haijabadilika, huku wanyakuzi wa ardhi wakidaiwa kula njama na maafisa wa ardhi ili kughushi stakabadhi za umiliki.

Uamuzi wa hivi majuzi wa mahakama ambapo ardhi ya mfanyibiashara mmoja jijini humo ilikuwa imenyakuliwa kwa kutumia stakabadhi ghushi imeibua suala hilo upya.

Mnamo Mei 19, Jaji Jane Muyoti Onyango, aliamuru kuwa mlalamishi, Bw Geoffrey Kipkemboi Lelei, ndiye mmiliki halali wa ardhi hiyo na kuamuru Msajili wa Ardhi wa Kaunti kusajili ardhi hiyo kwa jina la mlalamishi.

Visa kama hivyo vimekuwa vya kawaida jijini humo hasa katika mtaa wa Kipkaren, ambapo madai yametolewa kwamba mwanasiasa wa eneo hilo anadhibiti umiliki wa ardhi katika mtaa huo kwa kutumia wahuni kuwafurusha wamiliki halali.

Kesi ya hivi punde zaidi ni ambapo mnamo Jumatatu mfanyabiashara maarufu wa Eldoret, Bw Hosea Kibet Ruto, alishtakiwa kwa makosa tisa kuhusiana na ulaghai wa ardhi ya mamilioni ya pesa.

Bw Ruto ambaye alifikishwa mbele ya hakimu mkuu wa Eldoret, Bw Dennis Mikoyan, alikanusha mashtaka yote tisa.

Upande wa mashtaka uliambia mahakama kuwa unalenga kuwasilisha kortini mashahidi zaidi ya 20.

Mahakama ilimuachilia kwa dhamana ya Sh500,000 na dhamana mbadala ya pesa taslimu Sh200,000.

Kesi hiyo itatajwa Agosti 25 mbele ya hakimu mkuu mwandamizi, Bw Mogire Onkoba kwa maelekezo zaidi.

Kwa mujibu wa watetezi wa haki za kibinadamu katika ukanda wa North Rift wakiongozwa na Bw Kimutai Kirui kutoka Centre Against Torture, kesi hizo zinaonyesha bayana namna uovu na ufisadi umekita mizizi katika sekta muhimu ikiwa ni pamoja na idara ya ardhi miongoni mwa sekta nyingine.

“Kesi hizi zinaangazia haja ya kuchukuliwa hatua za haraka kukabiliana na unyakuzi wa ardhi na ufisadi katika Kaunti ya Uasin Gishu,” alisema Bw Kirui.

Hivi maajuzi waziri wa zamani wa elimu katika kaunti hiyo Bw Elijah Kosgei alisimulia jinsi jinamizi la ufisadi limekitia mizizi katika utawala wa kaunti hiyo.

Bw Kosgei alisema magenge ya wafisadi yameteka nyara kaunti hiyo ambapo imekuwa vigumu kwa gavana Jonathan Bii kukabiliana na wahusika.

“Ufisadi umekuwa kitu cha kawaida katika kaunti hii, magenge ya wafisadi wamemteka nyara gavana Bii ambapo imekuwa vigumu kwa gavna huyo kujinasua kutoka kwa magenge hayo hasa genge la Mosoriot,” alisema Bw Kosgei.

Mbali na ufisadi jiji la Eldoret limekuwa likishuhudia ongezeko la visa vya ulaghai.

Hivi maajuzi Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen alilalamikia kukithiri kwa ulaghai na kuongezeka kwa matumizi ya dawa za kulevya jijini humo.

Waziri Murkomen alikiri kuwa jiji hilo limekuwa kitovu cha walaghai wanaolenga wakaazi.

Akizungumza kabla ya kuhudhuria kika cha Jukwaa la usalama jijini humo mwezi jana nje ya afisi ya Kamishna wa Kaunti ya Uasin Gishu, Murkomen alisema uchumi unaokua wa Eldoret umevutia walaghai ambao wanawalaghai wenyeji mamilioni ya pesa kupitia mikataba ghushi.

“Tuna udanganyifu mwingi unaoendelea katika jiji hili ambapo wanafunzi wengi, wazazi na wafanyabiashara wametapeliwa. Pia tuna ulaghai mwingi wa ardhi katika eneo hili,” Murkomen alisema.

Waziri huyo aliagiza vyombo vya usalama kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wanaohusika na utapeli huo.

“Ninawahimiza wakazi kufikiria mara mbili wakati dili inapoonekana kuwa nzuri sana ili kujiepusha na walaghai ambao hujifanya wazuri kumbe ni wanaleng akuwatapeli. Daima tafuta ushauri wa kisheria au uwasiliane na afisi za serikali kabla ya kujitolea kufanya biashara au mikataba ya elimu,” alisema waziri Murkomen.