Wakoloni waliponyang’anya Jomo Kenyatta ardhi yake
KATIKA mojawapo ya visa vya kihistoria vilivyodhihirisha unyanyasaji wa mkoloni dhidi ya wapiganiaji wa uhuru, aliyekuwa Baba wa Taifa Mzee Jomo Kenyatta alinyang’anywa ardhi na kubomoa nyumba yake na Serikali ya Uingereza, muda mfupi baada ya kutangazwa kwa hali ya hatari nchini Kenya mwaka 1952.
Kenyatta, ambaye baadaye aliongoza taifa la Kenya kupata uhuru, alihukumiwa Aprili 8 1953 katika kesi ya kihistoria ya Kapenguria kwa tuhuma za kuongoza na kuwa mwanachama wa kundi haramu la Mau Mau. Alifungwa miaka saba na kazi ngumu.
Kwa kutumia sheria ya kutwaa ardhi ya 1953, Gavana wa wakati huo Evelyn Baring alitoa amri ya kutaifisha ardhi ya Kenyatta.
Kulingana na notisi rasmi ya Serikali nambari 1444 ya Oktoba 2 1954, vipande vinne vya ardhi ya Kenyatta huko Kiambu, vyenye ukubwa wa ekari 31.24, vilitwaliwa rasmi. Vipande hivyo vilikuwa vya ekari 2.9, 1.52, 11.06 na 15.76.
Kilichofuata kilishtua wengi. Serikali ilivamia boma la Kenyatta katika kijiji cha Ichaweri na kubomoa nyumba yake mawe kwa mawe.
Kila tofali lilichukuliwa hadi Gatundu, ambapo lilitumika kujenga nyumba ya serikali ya watumishi wa umma. Nyumba hiyo baadaye ikawa makazi ya viongozi wa utawala wa kikoloni eneo hilo.
Kwa mujibu wa aliyekuwa Kamishna wa Polisi Bernard Njinu, hatua hiyo ilizua matatizo kwa serikali ya mkoloni miaka minane baadaye, iliposhindwa kumshawishi Kenyatta kuhama Ichaweri alipokuwa karibu kuachiliwa kutoka gerezani mwaka 1961 anakumbuka Njinu, ambaye wakati huo alikuwa afisa wa kijasusi huko Isiolo.
Kenyatta, ambaye tayari alikuwa amechaguliwa kuwa kiongozi wa KAU bila kuwepo, alisisitiza kuwa hangefurahia uhuru wake iwapo hangerudi kwa ardhi yake mwenyewe. Hali hiyo ilipelekea serikali kuanza msako wa kumtafuta mtu aliyekuwa amepewa ardhi hiyo.
Njinu alielekezwa Gatundu na kufanikiwa kumfuatilia mmiliki mpya hadi Ngong, ambapo serikali ilifanikiwa kurudisha ardhi hiyo kwa Kenyatta.
Wanasiasa mashuhuri kama Masinde Muliro, John Keen na Wafula Wabuge walihusika kwa karibu katika kuhakikisha nyumba mpya inajengwa kabla ya kuachiliwa kwa Kenyatta.
Kenyatta aliachiliwa rasmi Agosti 14 1961, akapokelewa Kahawa na kusafirishwa hadi nyumbani Gatundu akiwa ameandamana na mkewe Mama Ngina, ambaye wakati huo alikuwa mjamzito.
Mtoto aliyekuwa tumboni alikuja kuitwa Uhuru, ambaye baadaye alihudumu Rais wa nne wa Kenya kuanzia 2013.
Kwa mujibu wa Njinu, siku ya kurejea kwa Kenyatta ilikuwa ya wasiwasi miongoni mwa baadhi ya wakoloni waliokuwa na hofu kwamba angechochea wafuasi wake dhidi yao.
Vile vile, walikuwepo ‘walinzi wa nyumbani’ waliowahi kushirikiana na wakoloni, waliogopa kulipizwa kisasi.
Njinu alikumbuka hadithi ya Ndung’u Kagoi, mshirika wa wakoloni kutoka Gatanga, ambaye aliposikia Kenyatta ameachiliwa huru, alifokea redio huku akiichapa kwa fimbo: “Gatutu gaka githi towe wanjirire ndakarekio na riu wandira magego wanjiira niarekio? Ndigithiria muchene!” (Redio hii! Wewe ndiye ulinambia Kenyatta amefungwa maisha, sasa unasema yuko huru? Acha porojo!)
Ili kumlinda Kenyatta, serikali ililazimika kuweka ua wa waya wenye misumari kuzuia umati wa wananchi waliokuwa wakimiminika kila siku kumuona. Kenyatta angewahutubia akiwa upande mwingine wa ua, akiwa amevalia koti lake la ngozi na kushika mgwisho wake.
Kwa kushangaza, Njinu aliishia kuishi kwenye nyumba iliyojengwa kwa kutumia mawe ya nyumba ya Kenyatta, baada ya kuhamishwa kuwa sehemu ya kikosi cha kumlinda Rais mwaka 1964. Baadaye, Kenyatta mwenyewe alimwamuru ahamie nyumba ndogo, ili daktari wake apatiwe ile kubwa zaidi.
“Kenyatta alijua fika kuwa nyumba ile ilikuwa ya mawe yake. Lakini kwa mtazamo wake wa ‘samehe lakini usisahau’, hakulifanya kuwa jambo la mzozo,” alisema Njinu.
Njinu aliendelea kumhudumia Kenyatta kwa miaka 14 hadi alipofariki dunia mnamo Agosti 22, 1978. Baadaye aliteuliwa kuwa Kamishna wa Polisi mwaka 1982 baada ya jaribio la mapinduzi ya kijeshi.