Nadco: Raila na Ruto walivyoacha Kalonzo kwa mataa
Ingawa Kalonzo alikuwa mstari wa mbele kuongoza mazungumzo yaliyolenga kutuliza joto la kisiasa nchini baada ya maandamano ya upinzani, hatua za hivi karibuni kutoka Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga zinamuacha nje ya utekelezaji.
Ripoti ya NADCO ilikabidhiwa rasmi Rais William Ruto na Raila Odinga ambao chini ya Serikali Jumuishi inayoleta pamoja vyama vyao vya UDA na ODM wameunda jopo la watu watano kufanikisha utekelezaji huku Kalonzo akiwa kimya na kutojumuishwa waziwazi katika vikao na hafla zinazohusu mchakato huo.
Baadhi ya wadadisi wa kisiasa wanaamini kuwa Kalonzo ameachwa kando kwa makusudi kutokana na msimamo wake wa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.
“Ni jambo la kushangaza kuwa mtu ambaye aliongoza mazungumzo haya kwa miezi mingi, sasa hashirikishwi katika mipango ya utekelezaji. Hii ni dalili ya siasa chafu za miungano ya kisiasa,” anasema mchambuzi wa siasa, Dkt Joseph Mutie.
Kuna tetesi kwamba Kalonzo aliachwa nje kwa kuendelea kukosoa ndoa ya kisiasa katika ya Raila na Ruto na ukuruba wake na aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua ambaye amekuwa akipondwa na vinara hao wa serikali jumuishi.
Washirika wake wengine katika upinzani akiwemo kiongozi wa DAP- Kenya Eugene Wamalwa na Martha Karua wa PLP, walitilia shaka NADCO wakisema haikuhusu maslahi ya raia wa kawaida.
“Kalonzo amekuwa mwepesi kukubali maridhiano, lakini hana nguvu ya kushinikiza utekelezaji wa matokeo ya majadiliano anayoyasimamia,” asema mchambuzi mwingine wa siasa Diana Kiango.Anasema kuachwa nje kwa Kalonzo katika utekelezaji wa Nadco ni sehemu ya mikakati ya Raila na Ruto kuelekea uchaguzi wa 2027.
“Inaonyesha ushirikiano wao ni wa kibaguzi na sio wa kuunganisha Wakenya wanavyodai. Utekelezaji wa ripoti ya mchakato wa kitaifa haufai kupunguzwa kuwa wa watu wawili au vyama teule vya kisiasa,” asema Kiango.Anasema utekelezaji wa ripoti hiyo unahitaji kushirikishwa kwa Wakenya wa matabaka yote.
Wafuasi wa chama cha Wiper wameanza kuuliza maswali kuhusu nafasi ya Kalonzo katika NADCO, wakihisi kuwa anapuuzwa licha ya kutekeleza jukumu kubwa katika ripoti hiyo.
“Tulifurahia Kalonzo kuwa mstari wa mbele katika mazungumzo ya NADCO. Lakini sasa tunashangaa kwa nini amepuuzwa wakati wa utekelezaji. Tunahitaji majibu,” alisema mbunge mmoja wa chama cha Wiper ambaye hakutaka kutajwa jina.
Kwa sasa, Kalonzo ameonekana kuchukua msimamo wa kimya kuhusu kutengwa kwake katika utekelezaji wa ripoti hiyo huku wachambuzi wakisema kuwa huenda anapima hali ya kisiasa.
Hata hivyo, kuna wanaohisi kwamba Raila na Ruto wamebadilisha suala muhimu la kitaifa kuwa la vyama viwili vya kisiasa.
Mutie asema kuna wale wanaodai kuwa Kalonzo bado ana nafasi ya kujijenga kama mgombea mkuu wa urais kwa tiketi ya upinzani, lakini kutengwa kwake katika utekelezaji wa ripoti hiyo iliyo na mapendekezo yanayohusu uchaguzi na utawala miongoni mwa mengine kunaweza kudhoofisha hadhi yake kitaifa.
“Licha ya juhudi zake kama mwenyekiti mwenza wa jopo hilo, anaonekana kupuuzwa kwa sasa na huu ni mkakati wa kisiasa wa kumfifisha kuelekea 2027 kwa msimamo wake wa kutojiunga na Serikali Jumuishi,” asema Mutie.