Makala

Masikitiko ya Gen Z Katiba iliyopitishwa wakiwa watoto baadhi wakiitaja ahadi hewa

Na NICHOLAS NJOROGE, CYNTHIA MAKENA August 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

WALIKUWA watoto wakati Wakenya walipopanga foleni mnamo mwaka wa 2010 kuupokea mwanzo mpya wa haki, ugatuzi na demokrasia.

Miaka kumi na tano baadaye, kizazi hiki cha Gen Z ndio wapiga kura wa kwanza walioishi maisha yao yote chini ya matumaini na pia masikitiko ya Katiba mpya.

Kutoka mijadala ya vyuoni hadi maandamano barabarani, kundi hili linafafanua upya maana ya uraia, na hawasiti kuwahoji viongozi wanaokiuka Katiba.

Miaka kumi na mitano iliyopita, katika siku yenye jua kali mwezi Agosti 2010, Wakenya walipiga kura kwa saa nyingi katika viwanja vya shule, kumbi za kijamii, na maeneo ya wazi, kupitisha Katiba mpya hati ya kisasa iliyoahidi haki zaidi, ugatuzi wa mamlaka, na haki.

Wakati huo, watoto wachanga waliobebwa mikononi na wanafunzi wa shule za msingi waliovaa sare zilizochakaa hawakuweza kuelewa kikamilifu uzito wa tukio hilo. Waliona tu furaha ya watu wazima, vidole vyenye wino, na vichwa vya habari kwenye magazeti vilivyotangaza: ‘Mapambazuko Mapya kwa Kenya.’

Leo, watoto hao wamekuwa watu wazima wa kizazi cha Katiba@15.

Wao ni wapiga kura, wanaharakati, wanafunzi, na wajasiriamali — kizazi cha kwanza cha kisiasa kilichoishi maisha yao yote chini ya Katiba ya 2010.

Kwao, Katiba si tu somo la uraia; ni kioo wanachotumia kutazama haki, utawala, na maana ya kuwa raia. Ni ahadi waliyoirithi, na ambayo wanaiweka kwenye mizani kila siku.

Nancy Jepkorir, mwanafunzi wa chuo kikuu mwenye umri wa miaka 21, hajawahi kuishi chini ya mfumo mwingine wa kisheria. Kwake, Katiba ni zaidi ya stakabadhi tu, anairejelea kila siku.

“Haki huvunjwa kila wakati, ingawa Katiba inaahidi haki kama ya kuishi na uhuru wa kujieleza,” asema kwa ujasiri wa kizazi chake.

“Sisi Gen Z tunajua Katiba kuliko vizazi vilivyopita. Tumeelimika zaidi na tuna ufahamu mkubwa wa yaliyomo. Lakini ukweli ni kwamba viongozi hawawajibiki kamwe. Ningekuwa na nafasi ya kubadilisha kitu kimoja, ningewaondoa wanasiasa wote wa zamani na kuanza upya.”

Kauli yake inaakisi mtazamo mpana wa kizazi kilichokuzwa si kwa kufundishwa haki tu, bali kwa kuzipigania moja kwa moja.

Kwa Vivian Kivuti, Katiba ilijiri na ahadi ya karibu na ya kipekee:

“Nililelewa nikiambiwa kuwa Kenya ina mojawapo ya Katiba za kisasa zaidi Afrika inayotoa ahadi ya usawa, haki, uwajibikaji, na ushirikishaji wa wananchi,” anakumbuka.

“Kwenye karatasi, ilikuwa na nguvu. Lakini kwa uhalisia, nimeshuhudia viongozi wakivunja sheria bila kuadhibiwa, wakitumia vibaya rasilmali za umma, na kupuuza haki ambazo Katiba inahakikisha.”

Anasema kizazi chake hakikujifunza Katiba kwa urahisi.

“Hatukufunzwa vizuri shuleni, tulilazimika kuielewa kujilinda. Mitandao ya kijamii, mijadala ya uraia, na uanaharakati vimetufumbua macho. Tunajua inachosema, na pia tunajua ni mara ngapi inapuuzwa.”

Kwa Brian Mugwimi, ambaye badala ya kupiga kura kwa mara ya kwanza mnamo uchaguzi wa 2022 alichagua kuwa karani wa uchaguzi, Katiba ni mwongozo wa vitendo.

“Kwa umri huu mdogo nilihisi napaswa kuanza kuelewa masuala ya uchaguzi na jinsi unavyoendeshwa,” asema.

“Kufanya kazi katika kituo cha kupigia kura kulinionyesha jinsi wapiga kura wanavyohamu kuchagua viongozi wanaowataka. Uchaguzi wa wazi huwapa watu imani kuwa viongozi wamechaguliwa, si kuteuliwa.”

“Nilijifunza kutii sheria na kuhakikisha haki. Ningependa kuona teknolojia ya hali ya juu zaidi katika uchaguzi ujao ili kufanya iwe rahisi na kuvutia vijana.”

Katika mji wa pwani alikokulia, Sammy Oluoch anakumbuka maisha kabla ya ugatuzi, ambapo huduma zilikuwa mbali, na maafisa wa serikali walionekana kama watu wa mbali kule Nairobi.

“Kabla ya 2010, sehemu kama yetu zilisahaulika,” asema.

“Sasa, huduma ziko karibu na wananchi si kamilifu, lakini viongozi wanaonekana na kuwajibika zaidi.”

Sammy, aliyejiunga na maandamano dhidi ya Mswada wa Fedha mwaka jana, anaelewa pande zote mbili za ahadi ya Katiba.

“Muundo wake umeleta nidhamu kwenye uchaguzi na huduma lakini baadhi ya viongozi wameipotosha kwa maslahi yao binafsi.”

“Roho ya Katiba iko hai miongoni mwa wananchi, lakini taasisi zilizopaswa kuitekeleza mara nyingi huipuuza.”

Licha ya kujitolea kwao kwa Katiba, vijana hawa wanaelewa fika kuwa ahadi zake bado hazijatimizwa kikamilifu. Afya kwa wote, elimu bora, na maisha yenye staha bado ni ndoto kwa wengi. Rushwa, siasa za kikabila, na ukosefu wa uwajibikaji bado vinaitafuna jamii.

Na bado, tofauti na baadhi ya vizazi vya zamani vinavyoona Katiba kama ndoto isiyotimia, Gen Z wanaiona kama chombo hai cha kutumika, kujaribiwa, na ikibidi, kurekebishwa.