Habari za Kaunti

Mutai anavyopanga kujitetea Seneti baada ya kutimuliwa na madiwani

Na COLLINS OMULO August 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

GAVANA wa Kericho Erick Mutai anapania kutumia mbinu ya kuibua pingamizi za mwanzoni kuzuia kuondolewa kwake afisini miaka miwili kabla ya kukamilisha muhula wake rasmi.

Gavana huyo anayehudumu muhula wa kwanza, anayetarajia kubahatika kwa mara ya pili, kwa mara nyingine anadai kuwa Bunge la Kericho halikutimiza hitaji la uwepo wa angalau thuluthi mbili ya madiwani kabla ya upigaji wa kura kwa hoja ya kumtimua.

Kwa hivyo, anapania kuzuia kamati ya maseneta wote 67 kuchunguza mashtaka dhidi yake, Jumatano.

Kulingana na Dkt Mutai, hakukuwa na angalau madiwani 32 kati ya 47 wanaohitajika kupitisha hoja ya kumbandua afisini.Gavana huyo anadai kuwa anaungwa mkono na jumla ya madiwani 18.

Lakini mnamo Agosti 15, 2025, madiwani walipiga kura kielektroniki matokeo yake yakiwa kwamba madiwani 33 waliunga mkono hoja ya kumwondoa Dkt Mutai afisini.

Lakini, kupitia wakili Katwa Kigen, gavana huyo anapinga matokeo hayo, kwa kuwasilisha hati viapo vilivyotiwa saini na madiwani 18.Hii inafanana na hali ilivyokuwa Oktoba mwaka jana, pale Bw Kigeni alipoibua pingamizi sawa na hizo na kufaulu kushawishi maseneta kutupilia mbali hoja ya kumtimua Dkt Mutai.

Wakili huyo alisema kuwa Bunge la Kaunti ya Kericho halikutimiza hitaji la kikatiba kwamba hoja ya kumtimua gavana sharti iungwe mkono na angalau thuluthi mbili ya madiwani.Hii ina maana kuwa kati ya madiwani wote 47 katika bunge hilo, sharti 33 waunge mkono hoja kama hiyo.

Wakiongozwa na Naaman Rop, madiwani 18 sasa wanadai kuwa hawakushiriki katika shughuli ya upigaji kura kieletroniki na hivyo madiwani 33 hawakupiga kura ya “Ndio” kwa hoja hiyo.

“Hii ina maana kuwa madiwani ambao huenda walipiga kura ya “Ndio” ama “LA” kwa hoja hiyo ilikuwa 29 pekee. Madai kuwa madiwani 33 walipiga kura ya kuunga mkono hoja hiyo ni uwongo,” Bw Rop akasema katika hatikiapo chake.

Madiwani wanaopinga hoja hiyo wanataka orodha ya majina ya wale waliopiga kura, saa ambayo kura ilipigwa na rekodi ya jinsi kura hizo zilihesabiwa.Wanadai kuwa mfumo wa upigaji kura kielektroniki ulivurugwa na mitambo hiyo haikukingwa dhidi ya uovu huo.