Habari

Ruto atangaza Agosti 27 Katiba Dei, ingawa haitakuwa likizo

Na CHARLES WASONGA August 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

RAIS William Ruto ametawaza rasmi Agosti 27 kuwa Siku ya Katiba (Katiba Dei) kwa ukumbusho wa siku ambayo Katiba ya sasa ilizinduliwa mnamo Agosti 27, 2010.

Kwenye tangazo alilotoa Jumatatu, Agosti 25, 2025, asubuhi, Rais Ruto alisema kuwa siku hiyo itatumika kwa maadhimisho ya miaka 15 tangu Kenya ilipopiga hatua hiyo katika “safari yetu kidemokrasia.”

Aidha, kulingana na Rais, Katiba Dei itakuwa ikiadhimishwa kila mwaka.

Dkt Ruto anailezea Katiba ya sasa kama mojawapo ya sheria endelevu katika historia ya binadamu kwani imekita “moyo wa kikatiba, ugatuzi, usawa kimaendeleo na kulindwa kwa haki za kimsingi na uhuru.”

“Wakenya wanapaswa kukumbuka siku hii kwani inakumbusha kuwa ni wajibu wetu kuzingatia, kutunza, kulinda na kutekeleza Katiba hii,” Rais Ruto akaeleza.

Kiongozi wa taifa alisema kuwa siku hiyo itaadhimishwa kote nchini na katika mabalozi ya Kenya katika mataifa ya ng’ambo.

“Wakenya wote nchini na katika mabalozi yetu yote kule nje watatumia siku hii kujikumbusha wajibu wao wa kuzingatia yaliyomo kwenye Katiba kwa kuendeleza midahalo kuhusu uzingatiaji wa katiba, uongozi na utawala wa kisheria,” akaeleza.

Japo Katiba Dei haitakuwa siku ya mapumziko, Rais ameagiza kuwa asasi zote katika nguzo tatu za serikali na ngazi mbili za serikali, zikiwemo shule, zitaandaa na kushiriki shughuli za kuhamasisha raia ili “kuendeleza ufahamu wao kuhusu yaliyomo kwenye katiba.”