Mabadiliko ya Katiba yalivyorejesha mamlaka kwa mwananchi wa kawaida
KATIBA ya 2010 ilibadilisha kwa kiasi kikubwa mfumo wa utawala nchini Kenya kwa kuondoa mamlaka mikononi mwa wanasiasa wa tabaka la juu na kuyarejesha kwa wananchi wa kawaida.
Ikiwa miongoni mwa katiba za kisasa zinazopigiwa mfano duniani, hati hiyo ya kisheria ilianzisha mageuzi makubwa yaliyoweka ushiriki wa wananchi kuwa msingi wa maamuzi yote muhimu ya kitaifa.
Kwa wananchi, Katiba hiyo ilipanua nafasi ya kidemokrasia kwa kuwapa nguvu ya kushiriki moja kwa moja katika maamuzi yanayowahusu, ikiwa ni pamoja na masharti yanayowataka viongozi kufanya kura ya maamuzi kubadilisha kipengele kinacholindwa cha katiba.
Katiba pia ilihalalisha ushiriki wa umma kuwa sharti la lazima katika mchakato wa bajeti na utungaji sera.
“Ushiriki wa umma ni kanuni ya lazima ya utawala chini ya Katiba, lakini bado hatuna sheria ya kuwezesha utekelezaji wake. Hili linapaswa kushughulikiwa kwa haraka,” anasema Caroli Omondi, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge la Kitaifa ya Uangalizi wa Utekelezaji wa Katiba.
Sura ya 4 ya Katiba ilipanua haki za raia, ikiwapa wananchi uhuru wa kujieleza, kuungana, na kupata habari. Hii imewapa wananchi nafasi ya kuwawajibisha viongozi wao, ikiwemo maandamano ya amani wanapohisi kukosewa.
Kwa misingi hiyo, baadhi ya mapendekezo ya mabadiliko ya Katiba yaliyotokana na misukumo ya kisiasa kama vile mpango wa BBI ulioanzishwa na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta na Raila Odinga – yalikataliwa, mengine mahakamani.
Hata hivyo, kwa viongozi walio mamlakani, Katiba hii imeifanya Kenya kuwa miongoni mwa nchi zenye kesi nyingi dhidi ya serikali, karibu kila uamuzi wa serikali ukipingwa mahakamani. Rais William Ruto pia amekumbwa na changamoto hizi, ambapo baadhi ya sera za serikali yake zimepingwa mahakamani.
Hata hivyo, Rais Ruto Jumatatu alitaja Katiba ya Kenya kama ‘inayoangazia mwananchi’, akisema ilianzisha mabadiliko ya kweli katika mfumo wa utawala.
“Kupitishwa kwa Katiba ya Kenya 2010 ilikuwa hatua ya kihistoria, ikianzisha enzi mpya ya katiba, utawala wa kumlenga mwananchi, ugatuzi, maendeleo ya haki, ulinzi wa haki za msingi, na matumaini ya pamoja ya taifa lenye haki, usawa na ustawi kwa wote,” alisema Rais Ruto alipotangaza Agosti 27 kila mwaka kuwa Siku ya Katiba.
Kabla ya Agosti 27 2010, rais alikuwa na mamlaka makubwa juu ya Bunge na Mahakama. Lakini Katiba ya 2010 ilianzisha mfumo wa kuangalia na kusawazisha mamlaka, ukijumuisha Mahakama huru, usimamizi wa Bunge na mashirika ya ukaguzi. Vilevile, Katiba ilianzisha tume za kikatiba na kukomesha urais wa kiimla kwa kurejesha mamlaka kwa wananchi.
Katiba pia iliongeza idadi ya wabunge na kutenganisha Bunge na Ofisi ya Rais. Mabadiliko haya yaliweka misingi ya ugatuzi, mojawapo ya mafanikio makubwa zaidi ya Katiba ya 2010.
“Taasis nyingi zilihisi kunyanyaswa na kukandamizwa chini ya Urais. Siku hizo hata Mahakama haikuwa huru; majaji waliteuliwa na Rais bila kushauriana na mtu yeyote. Sasa hali ni tofauti – tuna Hazina ya Mahakama inayoiwezesha kujisimamia. Polisi walikuwa idara chini ya Ofisi ya Rais, sasa ni taasisi huru,” alisema Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula.
Kuanzishwa kwa kaunti 47 kulitakiwa kusambaza rasilmali karibu na wananchi. Ugatuzi umekuwa mabadiliko yanayokumbatiwa sana licha ya changamoto zilizopo kwa baadhi ya taasisi mpya.
“Watu walioko mbali na Nairobi walikuwa wakisema ‘tunatoka Turkana tunaenda Kenya’ walipokuwa wakielekea Nairobi. Lakini sasa mambo yamebadilika – mamlaka ya kifedha na ya kutunga sheria yamepelekwa kwenye mabunge ya kaunti,” alisema Bw Wetang’ula.
Ugatuzi umeleta mabadiliko makubwa zaidi ya kijamii na kiuchumi, kwa kuwezesha rasilmali za kitaifa kusambazwa kwa usawa zaidi. Hata hivyo, changamoto bado zinazuia wananchi kunufaika kikamilifu.
Kwa mujibu wa Diana Gichengo, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la The Institute for Social Accountability (TISA), ugatuzi ulikuwa ‘mabadiliko makubwa kutoka utawala wa zamani’ kwani wananchi sasa wanahudumiwa moja kwa moja mashinani.