Patachimbika: Washirika wa Rais kugongana uchaguzi mdogo Mumbuni Kaskazini
WANDANI wa Rais William Ruto wanatarajiwa kutifuana kisiasa huku UDA na Maendeleo Chap Chap zikiwasilisha wawaniaji kwenye uchaguzi mdogo wa wadi ya Mumbuni Kaskazini, Kaunti ya Machakos.
UDA na MCC zote zipo kwenye mrengo wa Rais Ruto na iwapo mgawanyiko wa sasa utaendelea kushuhudiwa, basi huenda wakabwagwa kwenye uchaguzi huo na Wiper.
Katibu Mkuu wa UDA Hassan Omar na Katibu Mtendaji wa chama Vincent Musau ‘Kawaya’ walimtambulisha Misi Mutua kama mwaniaji wao wa Mumbuni Kaskazini.
Mfanyabiashara huyo wa Machakos alikuwa awali akivizia tikiti ya Wiper wakati ambapo UDA ilikuwa imeamua mfanyabiashara Job Nyumu awe mwaniaji wake.
Kabla ya Omar na Musau kumtambulisha Bw Mutua kama mwaniaji wa UDA, Bw Nyumu aliita kikao na kutangaza kuwa amejiondoa kwenye kinyang’anyiro na sasa atamuunga mkono Bw Mutua ashinde Mumbuni Kaskazini.
Kwa upande mwingine MCC nayo ilimtambulisha mfanyabiashara Harrison Wambua kama mwaniaji wake wadi ya Mumbuni Kaskazini.
Wiper pia haijaachwa nyuma katika uchaguzi huo wa Novemba 27 ambapo Antony Kisoi atapeperusha bendera yake.
“Wiper imeafikia kumuunga mkono Bw Kisoi,” akasema Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka alipomtambulisha rasmi mwaniaji huyo.
Bw Kisoi ana umri mdogo kuliko wapinzani wake ila Bw Mutua nayo anatoka eneo la Mungála ambako kuna kura nyingi.
Wachanganuzi wa masuala ya kisiasa nao wanahoji kwamba umaarufu wa chama utachangia mwaniaji kutamba kwenye uchaguzi huo.
Wadi ya Mumbuni imekuwa bila mwakilishi kutokana na mauti ya Gideon Kavuu miaka miwili iliyopita.
Wakati wa mazishi yake, Gavana wa Machakos Wavinya Ndeti alijitangaza kuwa diwani wa eneo hilo hadi mwengine achaguliwe.
MCC imekuwa ikisisitiza kuwa kiti hicho ni chao kwa kuwa marehemu Kavuu alikishinda kupitia chama hicho.
Bw Wambua naye alianza kampeni baada ya kuidhinishwa na Waziri wa Leba Alfred Mutua ambaye ni mwanzilishi wa MCC.
Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengu Mutuse ambaye pia ni wa MCC amekuwa akimpigia pia Bw Wambua kampeni kali huku akisisitiza kuwa ana imani watakishinda kiti hicho.
Ubabe kati ya wawaniaji wa UDA na MCC huenda kukasababisha wapoteze kiti hicho cha Wiper kwa urahisi.
Uhasama huo unahusishwa na vita vikali kati ya Bw Mutua na Kawaya ambao wote wanataka waonekane na Rais William Ruto kama wanaodhibiti siasa za Ukambani.