Wavuvi 24 wa Kenya wanyakwa na polisi wa Uganda Ziwa Victoria
LICHA ya juhudi za serikali kumaliza visa vya mara kwa mara vya kukamatwa kwa wavuvi wa Kenya na maafisa wa usalama wa Uganda, visa hivyo bado vinaendelea kushuhudiwa katika Ziwa Victoria.
Katika kisa cha hivi punde wavuvi 24 walikamatwa baada ya boti zao kuvuka mpaka wa kimataifa na kuingia ule wa nchi jirani.Boti sita za uvuvi pia zilinyakwa katika kisa hicho cha Jumatano usiku.
Wavuvi waliokamatwa walikuwa wametoka kisiwa cha Ringiti kilicho katika eneo la Suba Magharibi mapema siku hiyo kwa shughuli za uvuvi, wakiwa na nia ya kuuza samaki wao Alhamisi asubuhi.Hata hivyo, walikumbana na boti ya kushika doria za usalama ya Uganda.
Kulingana na mwenyekiti wa Chama cha Usimamizi wa Ufuo wa Kisiwa cha Ringiti, Bw Barnabas Odhiambo, wavuvi hao walizuiliwa kwa tuhuma za kuvuka mpaka bila idhini na hivyo kuingia nchini Uganda kinyume cha sheria.
“Ziwa hili ni kubwa na halina alama za kuonyesha iwapo mvuvi amevuka mpaka kuingia nchi nyingine,” alisema Bw Odhiambo.Alieleza kuwa wavuvi hao walikuwa wamegawanyika katika makundi mawili, kila moja likiwa na boti tatu.
Kukamatwa kwa 24 hao kuliibua taharuki miongoni mwa makundi ya wavuvi, ambao sasa wameomba serikali kuchukua hatua za haraka kuhakikisha Wakenya hao wanaachiliwa.
Baada ya kukamatwa, wavuvi hao pamoja na boti zao walipelekwa hadi Kisiwa cha Lolwe nchini Uganda. Wavuvi wengine walilazimika kusitisha shughuli zao za siku iliyofuata ili kutafuta njia ya kuokoa wenzao.
“Tumewahi kujikuta katika hali kama hii awali na tukalazimika kulipa faini kubwa ili kuachiliwa. Kiasi cha pesa hutofautiana. Tumaini letu sasa liko kwa serikali kuhakikisha wavuvi hao wanaachiliwa,” alisema Bw Odhiambo.
Kaimu Kamishna wa Kaunti ya Homa Bay, Bw Charles Mwayaya, alisema hana taarifa zozote.“Sijafahamishwa kuhusu tukio hilo. Hakuna malalamishi rasmi yamewasilishwa kwetu.
Lakini nitawasiliana na Mamlaka ya Ulinzi wa Pwani za Kenya (KCGS) kujua kama ina habari zozote,” akaeleza afisa huyo wa utawala.Hakuna takwimu za dhati kuhusu idadi ya wavuvi wa Kenya ambao wamekamatwa na Uganda, lakini si mara ya kwanza Wakenya kujikuta wakiwa korokoroni nchini humo.
Aidha, wavuvi hulalamika kudhulumiwa na maafisa wa usalama wa nchi hiyo jirani.Mara kwa mara, wavuvi kutoka Siaya, Migori na Homa Bay hujikuta wamekamatwa nchini Uganda wanapovuka mpaka kufanya shughuli za uvuvi.
Wakati wa kongamano la Uchumi wa Baharini lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Tom Mboya mjini Homa Bay mnamo Mei 30 mwaka huu, Rais William Ruto aliiagiza KCGS kuhakikisha wanawalinda wavuvi wa Kenya ziwani.
Dkt Ruto alisema kuwa kudhulumiwa kwa wavuvi ni moja ya changamoto ambazo serikali yake inalenga kutatua.Ili kupunguza migogoro, Rais alipendekeza kuanzishwa kwa sheria ya pamoja inayosimamia uvuvi katika mataifa matatu ya Afrika Mashariki – Kenya, Uganda na Tanzania.
“Majadiliano kuhusu hili yako katika ngazi ya mawaziri. Baadaye tutayapeleka katika ngazi ya marais kuhakikisha tuna sheria zinazofanana,” alisema Rais Ruto.Akiwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rais alisema atatumia nafasi hiyo kusukuma suala hilo mbele kwa kasi.
Kiongozi wa ODM Raila Odinga alitoa wito wa kutatuliwa kwa mvutano unaozingira umiliki wa Kisiwa cha Migingo, ambao umesababisha mizozo mingi kati ya wavuvi wa Kenya na polisi wa Uganda
“Tukubaliane na Uganda tujue mpaka uko wapi. Tunaweza pia kuwa na polisi wa majini ziwani ili kuhakikisha wavuvi wetu hawasumbuliwi,” alisema Waziri Mkuu huyo wa zamani wakati wa kongamano hilo.
\Bw Odinga alisema visa vya migogoro ni nadra sana katika Bahari ya Hindi, licha ya kuwepo kwa watu kutoka nchi mbalimbali ikiwemo za Bara la Asia.’Hali hiyo hiyo inapaswa kuwa Ziwa Victoria. Wavuvi wafanye kazi yao bila kuingiliwa,’ aliongeza.