Trump abatilisha uamuzi wa Joe Biden uliompa Kamala Harris ulinzi
RAIS Donald Trump ameondoa mpango wa kumpa ulinzi aliyekuwa Makamu wa Rais Kamala Harris uliowekwa na Joe Biden kabla ya kuondoka afisini Januari 20 mwaka huu.
Kama makamu wa rais wa zamani, kisheria, Bi Harris alipaswa kupewa ulinzi na serikali kwa muda wa miezi sita baada ya kuondoka afisini; kipindi kilichotamatika Julai, 2025.
Lakini muda huo uliongezwa kwa muda wa mwaka mmoja zaidi kupitia agizo lililotiwa saini na bosi wake wa zamani, Biden.
Lakini agizo hilo lilibatilishwa na Trump kupitia memoranda iliyotolewa Alhamisi.
Hatua hiyo inajiri kabla ya Harris kuanza kampeni ya kuvumisha wasifu wake “107 Days” kinachoangazia maisha yake kama makamu rais na kampeni yake ya urais 2024.
Barua ya Trump iliyoandikwa Agosti 28, 2025 inaagiza Idara ya Usalama wa Ndani “kusitisha usalama kwa Harris ndani ya muda uliozidi ule unaohitajika kisheria”.
“Utekelezaji wa agizo hili unapasa kuanza Septemba 1, 2025,” ikaeleza barua ya Trump.
Duru zilisema kuwa uchunguzi uliendeshwa juzi unaonyesha kuwa hamna hatari ambayo inaweza kuchangia kuongezwa kwa muda wa kutolewa kwa ulinzi kwa Harris zaidi ya muda wa miezi sita uliowekwa na sheria.
Mnamo 2008, Bunge la Congress lilipitisha sheria inayoiruhusu Idara ya Usalama kutoa ulinzi kwa makamu rais wa zamani, wachumba na watoto wao wenye umri usiozidi miaka 16.
Ulinzi kwa mumewe Harris, Doug Emhoff, ulitamatishwa mnamo Julai 1, baada ya kuisha kwa muda wa miezi sita unaotolewa na sheria.