Wabunge Indonesia wakubali marupurupu yakatwe kutuliza ghasia za Gen Z
JAKARTA, Indonesia
VYAMA vya kisiasa nchini Indonesia vimekubali kupunguza mishahara ya wabunge wao ili kusitisha maandamano kote nchini humo, Rais wa nchi hiyo Parbowo Subianto amesema.
Miji kadhaa katika taifa hilo la kusini mwa bara Asia, ikiwemo jiji kuu Jakarta, imeshuhudia maandamano kwa muda wa wiki moja iliyopita; ambayo imechangia makabiliano kati ya polisi na raia.
Japo, maandamano hayo yamechochewa na masuala kadhaa, ikiwemo kifo cha mwendesha pikipiki ya uchukuzi wa abiria, lalama kuu ni kuongezwa mwa marupurupu ya kila mwezi ya wabunge.
Jumapili Rais Subianto alitangaza kuwa viwango vya aina mbalimbali ya marupurupu vitapunguzwa.
Kiongozi huyo, ambaye amefutilia mbali ziara yake nchini China kutokana na machafuko hayo alisema baadhi ya waandamanaji hawakudumisha amani na wanaweza kuchukuliwa kama wanaoshiriki “uhaini au ugaidi.”
Rais Subianto aliongeza kuwa ameamuru polisi na wanajeshi kuzuia uporaji na uharibifu wa mali.
Boma la Waziri wa Fedha wa Indonesia ni miongoni mwa yale yaliyoporwa Jumapili, kulingana na vyombo vya habari.
Kimsingi, maandamano hayo yalichochewa na hatua ya kuongezwa kwa marupurupu ya wabunge kwa dola 3,030 (Sh393,900) karibu mara 10 ya mishahara ya chini zaidi jijini Jakarta.
Lakini maandamano hayo yaliongezeka zaidi kufuatia tukio la Alhamisi pale Affan Kurniawan, 21 alipogongwa na gari la polisi jijini Jakarta.
Mnamo Ijumaa watu watatu waliuawa baada ya waandamanaji kuteketeza jengo la bunge la jimbo.
Maandamano yaliendelea wikiendi hali iliyowalazimisha polisi kufyatua vitoza machozi kuwatanya waandamanaji.