TAHARIRI: Vinara waache MCAs wafanye maamuzi huru
MADIWANI wanastahili kutekeleza majukumu yao kwa uwazi na kwa kuzingatia katiba badala ya kuongozwa na tamaa.
Wakati huo huo, madiwani wanapaswa kuachwa kutekeleza majukumu yao bila kuingiliwa na vigogo wa kisiasa nchini.
Katika tukio la hivi punde, imebainika kuwa, juhudi zinaendelezwa na Rais William Ruto na Kinara wa Upinzani Raila Odinga kumwokoa Gavana wa Nairobi, Johnson Sakaja mikononi mwa madiwani.
Gavana huyo anakodolewa macho na shoka kutoka kwa madiwani ambao wamelalamikia utendakazi wake duni.
Hata hivyo, Raila na Ruto mnamo Jumanne walikutana na madiwani na kuwashawishi wasimwondoe Bw Sakaja madarakani.
Kwanza kabisa, ni vyema ifahamike kuwa, iwapo madiwani kwa kweli wana madai mazito kuhusu utendakazi wa Bw Sakaja, basi wanafaa waruhusiwe waendelee na mpango wao wa kumvua mamlaka.
Sheria inaruhusu Bw Sakaja asikizwe na atakuwa na nafasi ya kujitetea mbele ya madiwani kabla ya kura ya kumngátua kupigwa.
Tayari madiwani 92 kati ya 143 katika Kaunti ya Nairobi wametia saini hoja ya kumbandua.
Hii ni idadi kubwa na zaidi ya mara mbili ya 41 inayohitajika ili hoja hiyo iwasilishwe katika Bunge la Kaunti.
Vivyo hivyo, hii ni zaidi ya theluthi mbili ya idadi ya madiwani wanaohitajika kumbandua Bw Sakaja.
Rais Ruto na Raila walistahili kuwaacha madiwani wapambane na Bw Sakaja na iwapo hana hatia basi atajitetea mbele ya Bunge la Seneti.
Kuna magavana ambao waliwahi kusingiziwa makosa na sheria kukosa kufuatwa katika kungólewa kwao na walipofika Seneti, walinusurika.
Gavana wa hivi punde ni Eric Mutai wa Kericho ambaye ilibainika sheria haikufuatwa na madiwani katika kumfurusha.
Nairobi imekuwa na changamoto nyingi – raia wamekuwa wakilalamika jiji ni chafu, wachuuzi wako kila mahali, mpangilio ni duni na uongozi wa Bw Sakaja hauna habari.
Pia kumekuwa na madai ya ubadhirifu wa fedha ambao madiwani sasa hawatakuwa na fursa ya kuthibitisha, baada ya vinara wa miungano miwili mikuu kuingilia kati.
Katika uzi huo huo, baadhi ya madiwani nao wanatumia nafasi zao kuwafumba macho magavana na hiyo haifai kamwe.
Mara si moja, gavana anapokataa kuridhia matakwa ya madiwani kuhongwa, anatishiwa na hoja ya kumwondoa madarakani.
Vivyo hivyo, madiwani hao hao wamekubali kutumika na magavana kuwapiga vita wapinzani wao wa kisiasa.