Nuksi inavyoandama kiti cha ugavana Nairobi
Kwa zaidi ya muongo mmoja tangu kuanzishwa kwa ugatuzi nchini Kenya, kiti cha ugavana wa Nairobi – jiji kuu la Kenya na kitovu cha uchumi – kimeonekana kuwa na mikosi badala ya mamlaka.
Tangu utawala wa Evans Kidero (2013-2017), uliokumbwa na misukosuko, kuporomoka kwa Mike Sonko, hadi presha zinazomkabili Gavana Johnson Sakaja kwa sasa, kuna taswira inayoibuka ya kiti hiki kuwa cha laana.
Kidero, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa kampuni kubwa, alichaguliwa kuwa gavana wa kwanza wa Nairobi chini ya mfumo mpya wa ugatuzi mwaka wa 2013. Hata hivyo, utawala wake ulikumbwa na migongano ya mara kwa mara na mitandao ya “mabwanyenye” waliokita mizizi jijini – kutoka kwa ukusanyaji wa takataka, unyakuzi wa ardhi hadi ukusanyaji wa mapato na uchukuzi.
Utawala wake mara nyingi ulilaumu mitandao ya wafanyabiashara kwa kuzuia utoaji wa huduma bora na mageuzi. Licha ya tajriba yake katika sekta ya kibinafsi, Kidero alionekana kuzama katika kashfa za ufisadi, huduma duni, na shinikizo za kisiasa. Katika uchaguzi wa 2017, alishindwa kutetea kiti hicho na kuondoka akiwa hana cha maana cha kuonyesha, huku sifa yake ikiwa imepakwa tope kwa madai ya usimamizi mbaya.
Baadaye mwaka wa 2018, Kidero alikamatwa kwa tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi, ulanguzi wa fedha na hongo.
Mike Sonko, aliyekuwa maarufu kwa mtindo wake wa maisha wa kifahari na mvuto wa kisiasa mashinani, alimshinda Kidero mwaka wa 2017 kwa kampeni ya kisiasa ya kupendeza umma. Hata hivyo, umaarufu wake uligeuka kuwa mzigo.
Utawala wa Sonko ulijaa uongozi wa kubahatisha, matamshi ya hasira mitandaoni, na migogoro ya hadharani na maafisa wa serikali ya kaunti na ile ya kitaifa. Alidai kuwa ‘deep state’ ilikuwa ikimhangaisha na alikataa kuteua naibu gavana kwa muda mrefu.
Naibu wake, Polycarp Igathe, alijiuzulu ghafla Januari 2018 baada ya miezi mitano tu, akisema: ‘Kwa heshima na bila chuki, najiuzulu ili nisivunje au kudharau kiapo changu kwa Wakenya, wakazi wa Nairobi na familia yangu.’
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Sonko alisaini makubaliano ya kuhamisha majukumu muhimu ya kaunti – kama afya, usafiri, na upangaji miji – kwa serikali kuu mwaka wa 2020, jambo ambalo baadaye alidai alilazimishwa.
Hatua hiyo ilisababisha kuundwa kwa Huduma ya Nairobi (NMS) iliyoongozwa na Meja Jenerali Mohamed Badi, hali iliyomfanya Sonko kuwa kiongozi wa jina tu.
Kufikia Desemba 2020, Sonko aliondolewa rasmi na Bunge la Kaunti na uamuzi huo kuthibitishwa na Seneti kwa tuhuma za matumizi mabaya ya mamlaka – na hivyo kuwa gavana wa kwanza wa Nairobi kuondolewa ofisini.
Wapinzani wake walimlaumu kwa kuhujumu NMS, naye alitaja huduma hiyo kuwa “mpango wa wizi”. Seneti ilithibitisha uamuzi wa kumtimua mnamo Desemba 17, 2020, baada ya zaidi ya thuluthi mbili ya madiwani (88) kupiga kura kumuondoa.
Kisha akaja Johnson Sakaja, mwanasiasa kijana, aliyeahidi enzi mpya ya heshima na maendeleo. Alichaguliwa mwaka wa 2022 kupitia muungano wa Kenya Kwanza. Kama watangulizi wake, Sakaja alikuta mji mkuu umejaa migogoro ya muda mrefu, mifumo iliyovunjika na mitandao yenye nguvu ndani ya jiji.
Ajenda yake ya ‘Tufanye Nairobi Ifanye Kazi’ ililenga kurejesha mpangilio, kuboresha miundombinu na kuboresha ukusanyaji wa mapato. Hata hivyo, chini ya miaka mitatu baada ya kuchaguliwa, Sakaja anakumbwa na msukosuko – si tu kutoka kwa mitandao hiyo, bali pia kutoka kwa Wawakilishi wa Wadi na baadhi ya wananchi.
Wakosoaji wake wanamtuhumu kwa usimamizi mbovu wa fedha, deni la kaunti linaloongezeka, na mtindo wa uongozi wa kujitenga ambao umemkosesha uungwaji mkono.
Madiwani wametishia kumbandua kwa sababu ya huduma duni na ukosefu wa ushauriano. Wengine wanadai kuwa Sakaja amejenga kundi lake la mtandao wa uporaji ndani ya kaunti.
Sakaja amesalia thabiti, mara kwa mara akidai kuwa wanasiasa fulani wanafadhili machafuko katika jiji. Lakini historia haionekani kumfaa.
Kwa mujibu wa mtaalamu wa masuala ya utawala, Joyce Kimani, kuna mwelekeo usioepukika: “Kila gavana huanza na ahadi kubwa, hupambana na maadui, wa kweli au wa kubuni, anatofautiana na washirika wake wa kisiasa, na hatimaye kumezwa na misukosuko ya ndani.”
Dkt Isaac Gichuki, mtaalamu wa siasa anayeishi Amerika, anakubaliana naye. ‘Kutoka kwa vita alivyopigwa Kidero, hadi kuporomoka kwa kishindo kwa Sonko, na sasa msukosuko unaomkabili Sakaja, kiti cha ugavana Nairobi kimekuwa moto katika siasa za Kenya.’
“Iwapo kiti hicho kimelaaniwa au kimejaa uozo wa kimfumo bado ni mjadala. Lakini ukweli ni huu: bila mageuzi makubwa ya kimuundo katika kaunti na vyombo vya usimamizi, kiti hicho kitaendelea kuwa kaburi la kisiasa kwa yeyote atakayekikalia,” anasema Dkt Gichuki.
Kwa mujibu wa Kimani, afisi ya juu zaidi Nairobi ambayo hapo awali ilionekana kama kilele cha mamlaka, imegeuka kuwa mtego wa kisiasa, kutoka kwa mapambano ya kimuundo yaliyomsumbua Kidero, hadi kuporomoka kwa kishindo kwa Sonko, na sasa shinikizo linalomkabili Sakaja – kiti cha gavana Nairobi kinaonekana kuwa na laana inayojirudia.