Hii North Eastern inaweza kuwa ‘Tharaka Nithi mpya’ kura za 2027?
HUKU usajili upya wa wapigakura ukitarajiwa kuanza rasmi mwishoni mwa mwezi huu, macho yote yataelekezwa ukanda wa Kaskazini Mashariki ambao viongozi wake wameapa kuhakikisha wakazi wanajisajili kwa fujo kumpigia Rais Ruto kura mnamo 2027.
Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) imetangaza kuwa usajili wa wapigakura utarejelewa mnamo Septemba 29.
Tangazo hilo lilikuja baada ya mchakato wa kuhakikisha tume ina makamishina, mwenyekiti na sekretariati, kukamilika.
Mnamo Februari 5, Rais William Ruto aliondoa masharti makali ambayo yalikuwa yakiwaandama wale ambao walikuwa wakisaka kitambulisho kutoka Kaskazini Masharti.
“Pale nyuma vijana, watoto waliulizwa maswali mengi wanaposaka vitambulisho kana kwamba wao si Wakenya wa kawaida. Kama kuna maswali yanaulizwa basi yaulizwe watoto wote wa Kenya kwa usawa,” akasema Rais Ruto.
“Ubaguzi wa kikabila ambao umekuwa ukiendelezwa kwenye kaunti za kaskazini mashariki na zile mpakani lazima uishe,” akaongeza Rais Ruto.
Kauli hii ilichemsha nyongo za baadhi ya viongozi wa upinzani ambao waliona kama njama ya Rais kuongeza kura zake baada ya kupoteza uungaji mkono wa Mlima Kenya.
Pia kumekuwa na hofu kuwa raia wa Somalia huenda wakaingia nchini na kujisajili kama wapigakura.
“Rais alikuja hapa na kuondoa sheria ya kibaguzi kwa wanaochukua kitambulisho. Ni moto si moto, mtampa muhula mwingine kwa kuondoa msasa mwingi kwa wanaochukua kitambulisho?” akauliza Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki alipozuru Kaunti ya Wajir mnamo Agosti 24.
Viongozi wa Kaskazini Mashariki wakiongozwa na Waziri wa Afya Aden Duale wameapa mara kadhaa kuwa mara hii eneo hilo litasajili wakazi wake kwa fujo ili kumchagua rais kwa muhula wa pili.
Kwa mujibu wa takwimu za IEBC katika uchaguzi wa 2022, kaunti ya Garissa ilikuwa na wapigakura 201,743, Wajir (207,758), Mandera (217,030) nayo Marsabit 166,912.
Aidha, wengi eneobunge la Kamukunji, Nairobi wana asili yao kaskazini mashariki na Somalia.
Kuonyesha kuwa kaskazini mashariki ni kitovu kipya cha siasa za 2027, IEBC mnamo Julai ilazimika kukanusha ripoti kuwa wapigakura wapya milioni 3.5 walikuwa wamesajiliwa eneo hilo kutokana na mageuzi kwenye sheria ya uhamiaji.
Mwenyekiti wa IEBC Erastus Ethekon, kwenye taarifa alikanusha kuwa usajili wa wapigakura ulikuwa ukiendelea, akisema shughuli hiyo ilikuwa imesitishwa kutokana na IEBC kutokuwa na makamishina wote.
Kwa mujibu wa mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Martin Andati, kaskazini mwa Kenya itakuwa ikifuatiliwa sana kutokana na semi za viongozi wake na hatua ya serikali kuondoa msasa wa kitambulisho.
“Tayari kuna dhana kuwa eneo hilo ni faraja kwa Rais baada ya kupoteza Mlima Kenya. Pia baadhi ya viongozi wa eneo hilo hata wamekuwa wakilalamika kudhulumiwa kitakwimu wakati wa sensa kwa hivyo, bila shaka idadi ya waliosajiliwa kama wapigakura itakuwa ikifuatiliwa kwa karibu na wanasiasa,” akasema Bw Andati.
Mahakama iliamrisha sensa ya 2019 katika kaunti za Wajir, Mandera na Garissa irudiwe baada ya viongozi kudai takwimu zilizotolewa zilikuwa za idadi ya chini kuliko ile halisi ya wakazi wa magatuzi hayo.