Kimataifa

Trump amkaripia Netanyahu kwa kulipua Qatar akisaka viongozi wa Hamas

Na REUTERS September 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

DOHA, QATAR

RAIS wa Amerika Donald Trump amemkemea waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kuhusu mashambulio yaliyotekelezwa na jeshi lake dhidi ya Hamas nchini Qatar.

Trump alisema alijaribu kulizuia shambulio hilo lakini ‘alichelewa’, akiongeza kwamba ni uamuzi uliopitishwa na Netanyahu na wala si yeye.

“Sijafurahishwa na hilo,” Trump alisema alipokuwa akiwasili kwenye mkahawa Washington.

“Tunataka mateka waachiliwe, lakini hatujafurahishwa na kile kilichotokea jana.”

Video iliyosambazwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii ilionyesha moshi mkubwa ukizuka kutoka eneo lililo karibu na makao rasmi ya mabalozi wa kigeni na zilipo pia ofisi za viongozi wa Hamas wanaoishi uhamishoni nchini humo.

Sauti ya milipuko ilisikika katika mji mkuu wa Qatar, Doha.

Hamas ilithibitisha kufanyika kwa mashambulio hayo, ikisema viongozi wake walikuwa wanakutana kujadili pendekezo la kusitisha mapigano lililotolewa na Rais Donald Trump ambalo walishalikubali.

Hata hivyo, kundi hilo la wanamgambo wa Kipalestina lilisema viongozi wake wote walikuwa wamenusurika kwenye mashambulio hayo.

Qatar, mpatanishi muhimu katika mazungumzo baina ya Israeli na Hamas katika kutafuta njia ya kuvifikisha mwisho vita vya Gaza, imesema itaendelea na majukumu yake ya upatanishi licha ya shambulio hilo.

Qatar ilirejelea shambulio hilo kama tendo la ‘uoga’.

Katika taarifa yake, msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni wa taifa hilo la Kiarabu, Majid al-Ansar, alisema uchunguzi wa kina ulikuwa umeanza kufuatia mashambulio hayo na taarifa kamili itatolewa baada ya uchunguzi huo kukamilika.

Hata hivyo, Amerika haikutoa kauli yoyote kuhusu mashambulio hayo, lakini ripoti zinasema Israeli ilikuwa imeijulisha Washington kabla ya kuyatekeleza.

Ubalozi wa Amerika nchini Qatar ulitoa tangazo la kuwataka raia wake nchini Qatar kujificha kwenye maeneo salama.

Awali, Trump alikuwa amewatishia Hamas kwamba kutokukubaliana na pendekezo lake la amani kungekuwa na matokeo mabaya kwao, kauli ambayo wengine wanasema inaashiria rais huyo ambaye anaiunga mkono Israeli alikuwa anafahamu kilichokuwa kinapangwa.

Chansela wa Ujerumani Friedrich Merz na waziri wake wa mambo ya nje Johann Wadephul wamesema shambulio la Israeli nchini Qatar halikubaliki.

Naye Waziri Mkuu wa Italia Georgia Meloni ameelezea masikito yake kwa Emir wa Qatar Tamim bin Hamad Al Thani na Qatar nzima, akisisitiza msaada wa Italia kwa juhudi zote za kuvifikisha mwisho vita vya Gaza.

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa jana lilifanya kikao cha dharura kujadili shambulio la Israeli dhidi ya maafisa wa Hamas nchini Qatar.