Kimataifa

Gen-Z wa Nepal wamweka kiongozi wao madarakani

Na REUTERS September 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KATHMANDU, NEPAL

VIJANA wa Gen-Z Alhamisi, Septemba 11, 2025 walimpa Kulman Ghising nafasi ya kuongoza serikali ya mpito ya taifa hilo kama waziri mkuu.

Mhandisi Ghising anaheshimiwa sana na kuonekana kama mtu safi na Gen-Z waliofurusha serikali nzima mnamo Jumanne.

Ghising alikuwa Mkuu wa Mamlaka ya Kusambaza Umeme na anaonekana kama alichangia sana katika uthabiti wa sekta hiyo.

Awali, Gen-Z walimkataa Jaji Mkuu wa zamani Shushila Karki wakimtaja kama kiongozi mzee na pia wakatilia shaka kufuzu kwake.

Kulikuwa na mgawanyiko kwa sababu mrengo mmoja ulikuwa ukimuunga Karki ambaye bado ameonyesha nia ya kuongoza taifa hilo iwapo uchaguzi utaandaliwa.

Tangazo hilo la Gen-Z linajiri huku vuguvugu la kupambana na ufisadi na kueneza uongozi bora, likiunga mkono kubuniwa kwa Baraza la Mpito kusaidia nchi hiyo kwenye mchakato wa kuwa na serikali thabiti.

Haya yanakuja wakati ambapo idadi ya vifo kutokana na maandamano hayo imefikia watu 31. Idadi hiyo ilikuwa watu 25.

“Tumefanya upasuaji na uchunguzi kwa miili mbalimbali lakini bado hatuwezi kuyatoa maelezo zaidi ya ufichuzi kwa jamaa zao,” akasema Dkt Gopal Kumar Chaudhary mkuu wa kitengo cha matibabu hospitalini Trtibhuyan.