Ghana pia yakubali Trump airushie wahamiaji haramu
ACCRA, GHANA
GHANA ‘imejificha’ nyuma ya Uafrika na kutangaza kuwa itawakubali wahamiaji haramu kutoka Amerika ambao wana asili ya Afrika Magharibi.
Kwa mujibu wa Rais wa Ghana John Dramani Mahama, tayari wahamiaji haramu 14 ambao walifurushwa kutoka Amerika wameletwa nchini humo.
Rais Donald Trump wa Amerika amekuwa hasimu mkuu wa wahamiaji. Amekuwa akiwahamisha wale ambao wako nchini humo kinyume cha sheria, wengi wakiwa wahalifu sugu.
Mara si moja Trump amekuwa akirai nchi za Afrika na mataifa mengine ambayo hayajaendelea yakubali kuwapokea wahamiaji hao ili nao wapokee tunu kutoka Amerika.
Mahama hakufafanua idadi ya wahamiaji haramu ambao Ghana wamekubali kuwapokea. Alijitetea akisema kuwa raia wa Afrika Magharibi hawahitaji visa ili kufika Ghana.
“Amerika ilituomba tukubali kuwapokea wahamiaji wanaofurushwa huku na wanatoka Afrika Magharibi. Tulikubali kuwapokea kwa sababu raia wote wa Afrika Magharibi hawahitaji visa ili kufika nchi yetu,” akasema.
Utawala wa Trump umekuwa ukifikia nchi za Afrika kuhakikisha kuwa inapunguza idadi ya wahamiaji haramu nchini humo.
Ingawa hivyo, baadhi ya wahamiaji wamelalamika kuhusu usalama wao, wengine hata wakiwa hawafahamu lugha ya nchi ambako wanapelekwa.
Mnamo Julai, Amerika iliwatuma wahamiaji watano hadi Eswatini na wengine wanane Sudan Kusini.
Rwanda iliwapokea wahamiaji saba kutoka Amerika mnamo Agosti wiki chache baada ya kuingia kwenye makubaliano ya kuwapokea wahamiaji 250.
Mnamo Julai 9, Trump aliwapokea marais watano kutoka Afrika Magharibi katika Ikulu ya White House.
Duru zinaarifu Trump alitumia mkutano huo kuwashawishi marais hao wakubali kuwapokea wahamiaji kutoka Amerika.