Akili MaliMakala

Wafugaji walivyoanzisha kampuni ya bidhaa za nyama

Na SAMMY WAWERU September 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KARIBU miaka mitano iliyopita, kundi la wakulima kutoka Kaunti ya Laikipia waliungana kwa lengo moja: kuziba pengo la upatikanaji wa nyama bora, salama na ya hadhi kwa masoko lengwa yao.

Laikipia, mojawapo ya kaunti kame na nusu-kame (ASAL) nchini, inategemea sana ufugaji na huchangia pakubwa katika sekta ya nyama nchini.

Hata hivyo, changamoto ya upatikanaji wa nyama salama kwa walaji bado ni kibarua, licha ya juhudi za serikali kupitia Mswada wa Usalama wa Chakula na Malisho wa 2023 – ambao upo katika awamu ya mwisho kupitishwa kuwa sheria.

Ni pengo ambalo wakulima-wafugaji kutoka Laikipia walitambua mwaka 2020, Kenya ilipothibitisha kuwa mwenyeji wa janga la Covid-19, na hapo ndipo kampuni ya Ongole Beef ilipozaliwa, ikilenga kuhakikisha walaji wanapata nyama ya ubora wa juu.

Vipande maalum vya nyama vinavyouzwa na Ongole Beef, kampuni iliyoko Laikipia. Picha|Sammy Waweru

“Ni mtoto wa Corona tunayejivunia,” anasema Eric Muriithi, Msimamizi wa Masoko ya Rejareja na Utafiti wa Soko, Ongole Beef.

“Janga la kimataifa lilipotukumba kama taifa, tuligundua kuwa upatikanaji wa chakula bora ni muhimu. Tukajitosa kuziba pengo hilo – la nyama.”

Ongole Beef inamiliki kichinjio cha kisasa Laikipia, na inasambaza vipande maalum vya nyama kama vile ribeyesirloinT-bone na tomahawk.

Muriithi anasema wameipa kipaumbele uwekezaji kwenye mifumo ya uhifadhi wa baridi na barafu, maghala na magari ya kusafirisha nyama.

“Ili kupata nyama laini, nyororo na iliyoafikia ubora, lazima mtayarishaji afuate viwango vilivyowekwa vya kitaifa na kimataifa vya nyama, kuanzia ufugaji, uchinjaji, uhifadhi nyama na usafirishaji. Tunafuatilia historia ya mifugo kuanzia kwa mmiliki,” anaongeza.

Eric Muriithi, Msimamizi wa Masoko ya Rejareja na Utafiti wa Soko, Ongole Beef akikagua bidhaa za nyama zinavyochomwa wakati wa maonyesho ya Kenya Meat Expo & Conference 2025, KICC Nairobi. Picha|Sammy Waweru

Hatua hiyo ni muhimu kwa masoko ya kimataifa, ambapo Kenya huuza nyama hasa katika nchi za Uarabuni, chini ya muungano wa Gulf Cooperation Council (GCC) kama vile UAE, Saudi Arabia, na pia mataifa ya Afrika Mashariki na Kati.

Mbali na kuwa na kichinjio cha kisasa, Ongole Beef ina sehemu maalum kufuga wanyama – feedlot, ambapo huboresha mifugo kabla ya kuchinjwa.

Feedlot, inatumika kuwapa chakula, madini na virutubisho faafu kwa minajili ya kuafikia viwango vya kitaifa na vya kimataifa vya nyama.

“Tunanenepesha mifugo kwa miezi michache tukiwapa chakula na madini, huku mavetinari wetu wakiwakagua kiafya,” anasema Muriithi. Wateja wao wakuu ni hoteli na mikahawa ya kifahari jijini Nairobi.

Soseji na burger zilizoundwa na Ongole Beef. Picha|Sammy Waweru

Baada ya miaka mitano kuwa kwenye mtandao wa nyama, kampuni hiyo inajivunia kupanua huduma zake.

Mwaka 2024, ilizindua utengenezaji wa nyama iliyoongezwa thamani, inayojulikana kama dry-aged meat, inayohifadhiwa kwa muda wa siku 21 hadi 45 kwenye mazingira yenye joto na unyevuunyevu unaodhibitiwa.

Hii hufanya nyama kuwa na ladha bora, laini na mwororo. “Taratibu za dry-aged meat zinasaidia kuboresha nyama na kuteka soko bora,” anafafanua Tito Sammy, Mkuu wa Mawasiliano ya Masoko.

Kwenye Makala ya Nne ya Kenya Meat Expo & Conference 2025, Ongole Beef ilizindua bidhaa mpya za nyama zenye thamani ya juu.

Bidhaa hizo ni pamoja na sausage za Ongole, beef macon, kebab za nyama zilizochanganywa na viungo, na bidhaa za nyama za kondoo.

Baadhi ya wafanyakazi wa Ongole Beef katika Makala ya Nne ya Kenya Meat Expo & Conference 2025, yaliyofanyika KICC, Nairobi. Picha|Sammy Waweru

Tito anasema, “Kuzindua bidhaa hizi ni hatua muhimu sana kwetu, hasa kwa minajili ya kuteka masoko mapya.”

Kenya Meat Expo huandaliwa na Shirika la Nation Media Group (NMG) PLC, na hafla ya mwaka huu ilivutia zaidi ya watu 10,000 na waonyeshaji 100.

Ilifanyika katika Ukumbi wa KICC, Nairobi, kati ya Agosti 6 na 8, na ilifunguliwa rasmi na Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo, Mutahi Kagwe, aliyetoa wito kwa sekta za kibinafsi kushirikiana na serikali kuboresha sekta-ndogo ya nyama.

‘Mpishi’ wa Ongole Beef wakati wa Makala ya Nne ya Kenya Meat Expo & Conference 2025, KICC, Nairobi, akichoma nyama na bidhaa za nyama. Picha|Sammy Waweru