Akili Mali

Malisho yanayostahimili tabianchi yanavyonisaidia kuongeza maziwa

Na SAMMY WAWERU September 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KWA zaidi ya miaka saba iliyopita, wafugaji wa ng’ombe wa maziwa nchini Kenya na Afrika Mashariki wamekuwa wakihangaika kutokana na gharama ya juu ya chakula cha mifugo, na Anthony Kiarie Muigai hajakwepa mjeledi huo.

Akiwa mkazi wa Kaunti ya Nyandarua, Kiarie anasema katika kipindi cha miaka 19 ya ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, hajawahi kushuhudia mahangaiko kama ya mwaka wa 2019 na 2020.

Kupanda kwa bei ya chakula cha mifugo cha madukani, uhaba wa malighafi kukiunda na ushuru na ada zinazotozwa, imekuwa kero kwa sekta ya ufugaji – suala linalochochea baadhi ya viwanda kupunguza kasi ya uzalishaji.

Inakadiriwa, Kenya huagiza zaidi ya asilimia 70 ya malighafi ya chakula cha mifugo nje ya nchi.

Anthony Kiarie akiwapa ng’ombe wake chakula. Picha|Sammy Waweru

Kiarie, hata hivyo, changamoto hizo anazikwepa kwa kukuza nyasi na mimea inayohimili athari za tabianchi, kama vile kiangazi na ukame.

“Ijapokuwa kuna changamoto nyingi zinazozingira sekta ya uzalishaji maziwa, kupitia malisho yanayostahimili mabadiliko ya tabianchi, hasa yale yenye protini na wanga (carbohydrates) nyingi, nimeweza kupunguza gharama ya uzalishaji kwa kiwango kikubwa,” anadokeza.

Kwenye shamba lake la ekari nne, na ekari 10 anazokodisha, Kiarie hulima malisho aina ya lucerne, mahindi, super Napier Pakchongvetch na viazi vitamu.

Anakuza aina ya mahindi ya PAN 691 kwenye ekari 10, mbegu inayosifiwa kuhimili kiangazi na inayokomaa kati ya siku 90 hadi 100.

Anthony Kiarie akiwa kwenye shamba la Lucerne. Picha|Sammy Waweru

Lucerne ninailima kwenye nusu ekari, huku viazi vitamu na vetch vikibadilishana na mimea mingine ninayokuza kwenye ekari nne ninazomiliki,” anaongeza mkulima huyo mwenye kandarasi na kampuni ya Brookside Dairy kuisambazia maziwa.

Kwa sasa Kiarie ana ng’ombe 12, nane wakizalisha maziwa. Aidha, shamba lake limekumbatia mfumo wa kutopoteza chochote, ndio ‘zero waste’ kwa Kiingereza, ambapo samadi hutumika kutengeneza gesi ya kupikia kupitia biodigester. Mabaki ya samadi hiyohiyo, hutumika kama mbolea na kufunika ardhi ili kuzuia kwekwe kumea.

“Haifanyi kazi tu kama mbolea, bali pia huzuia kwekwe dhidi ya kumea,” anaelezea.

Majani ya viazi vitamu ambayo Anthony Kiarie anatumia kupunguza gharama ya ufugaji. Picha|Sammy Waweru

Maamuzi yake kubadilisha malisho ulitokana na utafiti aliofanya.

Anakumbuka bei ya gunia la kilo 50 za chakula cha mifugo cha madukani ikipanda kutoka Sh2,200 hadi Sh2,450.

“Kwa mkulima anayehitaji kusalia kwenye biashara ya maziwa, lazima kuwe na mbinu mbadala za kupunguza gharama,” anasisitiza.

Mradi wa Nourishing Prosperity Alliance (NPA) Forage unaoendelezwa na NPA katika kaunti za Meru, Nyeri, Nyandarua, Nakuru, Kericho, Baringo, na Uasin Gishu, ulimsaidia kupata suluhu.

Masalia ya kinyesi yanayotumika kuzalisha biogasi Anthony Kiarie anayaelekeza shambani mwake. Picha|Sammy Waweru

“Gharama kubwa zaidi katika uzalishaji wa maziwa ni malisho. Wakulima wanahangaika kwa sababu bei ya chakula cha madukani ni ghali mno,” anasema Renny Chemtai, mtaalamu wa lishe ya mifugo NPA.

“Tunapendekeza kilimo cha lucerne, mahindi aina ya PAN 691 na PAN 9M-91, forage sorghum na pearl millet. Ni mazao yaliyosheheni protini, wanga na yanayostahimili mabadiliko ya tabianchi,” anaongeza Chemtai.

Baada ya miaka mitano ya kutumia malisho haya, Kiarie anasema gharama ya kuendeleza ufugaji wa ng’ombe wa maziwa imeshuka kwa asilimia 60.

Kinyesi kinachotumika kukuza Lucerne kwenye shamba la Anthony Kiarie. Picha|Sammy Waweru

“Hapo awali nilikuwa nikitumia kati ya kilo 10 hadi 12 za chakula cha madukani kwa ng’ombe mmoja kila siku. Sasa gharama imepungua pakubwa,” anasema.

Kila ng’ombe huzalisha kati ya lita 14 na 32 za maziwa kwa siku, na kwa jumla husambazia Brookside Dairy lita 200 hadi 300, ambayo hununua lita moja kwa Sh48.

Anafichua kwamba, kila ng’ombe ana bima ya Sh200,000. Kabla kuingilia ufugaji huo, Kiarie alikuwa akifanya vibarua jijini Nairobi.

Bwawa ambalo Anthony Kiarie hutumia kuvuna maji ili ayatumie kulima nyasi maalum za mifugo. Picha|Sammy Waweru