Makala

Mitandao ya wizi wa simu inavyotawala Nairobi

Na  JOSEPH WANGUI September 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

Mitaa yenye shughuli nyingi ya Nairobi inaficha uchumi wa uhalifu unaoendelezwa kwa ustadi—mitandao ya wizi wa simu inayojumuisha wanyang’anyi, wanunuzi, mafundi wa simu, na walanguzi wa kuvuka mipaka.

Licha ya misako mikali ya polisi katika Jiji Kuu ambayo imesaidia kurejesha zaidi ya simu 500 ndani ya mwaka mmoja uliopita, mitandao hii inaendelea kustawi kwa kutumia utaalamu wa kiteknolojia na soko haramu lisilo na kikomo.

Kukamatwa kwa washukiwa wakuu wanaohusishwa na mtandao hatari kati kati ya Nairobi kumefichua ukubwa wa biashara hii na kasi ya ongezeko la wizi wa vifaa hivyo.

Takwimu za polisi zinaonyesha kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, simu 574 zinazoshukiwa kuibwa zilipatikana na maafisa wa usalama jijini Nairobi wakati wa operesheni za kusambaratisha mitandao hiyo.

Mshukiwa aliyepatikana na simu 73 zinazodaiwa kuwa za wizi pia alidokeza uwepo wa mtandao uliosukwa vizuri na wenye vifaa vya hali ya juu vya kurekebisha na kuuza tena simu hizo.

Ripoti za awali za polisi zinaonyesha uwepo wa mtandao wa kuvuka mipaka baada ya kukamatwa kwa raia wawili wa kigeni na Wakenya wawili kati kati ya Nairobi wakiwa na kifurushi cha simu 13 aina ya smartphone zinazodhaniwa kuelekezwa  soko la magendo nchini Uganda.

Hili linaeleza kwa nini simu nyingi za kisasa huibwa na kutoonekana tena kabisa.

Licha ya operesheni nyingi dhidi ya wanyang’anyi na vibanda vya kutengeneza simu pamoja na simu nyingi kuwa zana za ufuatiliaji—wizi wa simu unaendelea nchini Kenya, kwani vifaa hivyo vina thamani kubwa.

Kwa mfano, Juni mwaka huu, maafisa wa polisi kutoka Nairobi walifanya oparesheni ya kijasusi katika Barabara ya Tsavo  na kupata simu 75 zinazodhaniwa kuibwa.

Walipata pia vifaa 20 vya Universal Flashing Interface (UFI) vinavyotumika kufuta na kurekebisha data katika simu.

Mwezi uliofuata, mshukiwa mmoja alikamatwa Mathare akiwa na simu 72 za wizi, na miezi miwili kabla yake mshukiwa mwingine alinaswa Naivasha akiwa na simu 27 zinazoshukiwa kuibwa.

Polisi walipata pia kifaa kinachotumika kurekebisha vifaa hivyo kabla ya kuviuza tena sokoni.

Vivyo hivyo, Mei mwaka huu, maafisa wa usalama walipata simu 77 katika Barabara ya Munyu na Mfangano, Nairobi, za thamani ya Sh614,000.

Kukamatwa kwa washukiwa zaidi kumeongezeka mwaka mmoja baada ya polisi kunasa simu 182 zinazoshukiwa kuwa za wizi katika duka la kielektroniki eneo la Ruai, Mei 2024.

Wakati wa operesheni hiyo, polisi walikamata pia simu nyingine 19 Kamukunji na 34 Lang’ata.

Katika kipindi hicho hicho, walipokuwa wakifuatilia simu ya wizi iliyochukuliwa kutoka kwa mwathiriwa Kilimani, maafisa walinaswa simu 42 kutoka duka la kutengeneza simu katika Barabara ya Kimathi, CBD.

Novemba 2022, maafisa wa DCI eneo la Kasarani walikamata simu 265 aina ya iPhone na simu nyingine 10 za Android kutoka kwa mshukiwa wa mtandao unaoendeleza wizi huo.

Kutokana na kukamatwa kwa washukiwa hao, imebainika kuwa mbali na wale wanaonyakua simu moja kwa moja, kuna wahusika wengine kama mafundi wa simu wanaosaidia kufuta data na kuziuza tena.

Mafundi hao huondoa taarifa za mtumiaji wa awali, kuharibu nambari za IMEI, na kubadilisha muonekano wa kifaa, na kufanya iwe vigumu kutambuliwa.

Wahusika wengine ni wataalamu wa IT wanaofungua simu zinazomilikiwa na mashirika ya kifedha ya kidijitali yanayotoa huduma kwa Wakenya.

Wauzaji wa simu hizo—kwa njia za mtandaoni au madukani—wanachangia pia kuendelea kwa soko hilo la magendo. Hivyo basi, wanachama wa mtandao huu wa uhalifu wamepata njia rahisi ya kuendeleza biashara hiyo bila kugundulika.

Mashirika kama M-Kopa, Watu Credit na Mophone Kenya, yanayotoa simu kwa mpango wa kulipia kidogo kidogo, yameathirika pakubwa kutokana na kufunguliwa kwa simu hizo kabla ya mikopo kukamilika.

Wahalifu wengine ni masoko ya mtandaoni yanayoruhusu uuzaji wa simu za wizi kwa siri, pamoja na wamiliki wa cyber cafe na wataalamu wa IT wanaozifungua simu za wateja kwa mkopo.

Washukiwa watatu kwa sasa wanakabiliwa na mashtaka ya kufungua simu za thamani ya Sh3 milioni za M-Kopa na Watu Credit kabla ya kumaliza mikopo yao.