Miili ya Kwa Binzaro ilitupiwa wanyama kuficha ushahidi, mahakama yaelezwa
UCHUNGUZI wa vifo vya dhehebu la Kwa Binzaro umechukua mkondo wa kutisha baada ya kubainika kuwa miili ya waathiriwa wengi ilitupwa msituni ili itafunwe na wanyama wa porini kwa lengo la kuharibu ushahidi.
Upande wa Mashtaka ulifichulia mahakama kuwa baadhi ya waathiriwa hawakuzikwa kabisa, bali mabaki yao yalitupwa kichakani huku mshukiwa mkuu akifikishwa kortini.Wengine walizikwa kwenye makaburi yasiyozidi futi moja kwa kina, hali iliyowaacha wakiwa mawindo ya wanyama.
“Idadi kubwa yao hawakuzikwa hata kidogo, walitupwa msituni na wakaliwa na wanyama wa porini. Makaburi hayakuwa ndani ya ekari tano za awali zilizokuwa zikichunguzwa,” alisema kiongozi wa mashtaka Jami Yamina.
Bw Yamina alisema kuwa uchunguzi unaondelea kufanyika unaonyesha kuwa huenda mili kadhaa ikapatikana katika makaburi ambayo yametambuliwa kuwa katika hekari 400 kutoka kwa ekari tano za awali.
Alibainisha kuwa kupatikan kwa viungo vya binadamu 102 ulikuwa ushahidi tosha kuwa wengi wa waathiriwa wa Kwa Binzaro hawakuzikwa ipasavyo bali walitupwa kichakani na kuliwa na wanyama.
Jana, Hakimu Mwandamizi wa Malindi Joy Wesonga aliagiza washukiwa wanne wawekwe chini ya ulinzi wa mashahidi baada ya maombi ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP).
Watakuwa mashahidi dhidi ya mshukiwa mkuu Sharleen Temba Anido, na washirika wake watatu.Wakati huo huo, mahakama iliamuru kuachiliwa kwa Safari Kenga Nzai, Karisa, Gona Fondo na Charo Gona Kalama kwa dhamana ya bure chini ya masharti makali, yakiwemo kuripoti mara kwa mara kwa maafisa husika.
Wakati huo, polisi waliomba siku 60 zaidi kuwazuilia Bi Anido, Kahindi Kazungu Garama, Thomas Mukonwe na James Kazungu, walioko katika vituo vinne vya polisi Kilifi.
Huku akitegemea stakabadhi za mchunguzi wa kesi hiyo Oliver Nabonwe , Bw Yamina alisema uchunguzi imewahusisha moja kwa moja washukiwa wa Kwa Binzaro na maafa ya Shakahola, ambako takriban wafuasi 454 wa mhubiri tata Paul Mackenzie wa kanisa la Good News International walifariki kutokana na kufunga kula kwa lazima.
Kwa mujibu wa Bw Yamina, wanne hao waliwashawishi na kuwapotosha wafuasi na kuendesha vifo walivyoviita “safari takatifu ya kumwona Yesu.“Hawa sio tu wanaweza kutoweka bali pia wanaweza kujiua wakati wowote wakipata nafasi,” alisema.
Hadi sasa, miili 34 na mabaki ya binadamu 102 yamepatikana katika msitu wa Kwa Binzaro. Sampuli za DNA zimekusanywa na mashahidi zaidi ya 50 wamehojiwa.Pia , uchunguzi umeonyesha kuwa makaburi Zaidi yanshukiwa kuwa katika ekari 400 katika kichaka hicho.Uchunguzi pia imefichua kuwa wote wanne waliwahi kuishi Shakahola.
Watoto watano wa Garama wako kwenye kituo cha kulelea watoto Kilifi, mke na watoto watatu wa Mukonwe wametoweka na wanahofiwa kufa, huku mke wa Kazungu akikabiliwa na mashtaka 238 ya kuua bila kukusudia mjini Mombasa na watoto wao watano wakiwa hawajulikani walipo. Mume wa Bi Anido pia anadaiwa kufa kutokana na Imani kali za kidini.
Msako majumbani mwao ulibaini kadi za simu 15, kadi ya kuhifadhi data , kitambulisho cha mmoja wa waathiriwa, jembe chafu linaloshukiwa lilitumika kuchimba makaburi msituni, mikataba ya ardhi na mkataba wa mauzo ya pikipiki (KMDD 554X) iliyodhaniwa kutumika kuwapeleka waathiriwa eneo la kufunga. Bw.Yamina alisisitiza kuwa maziko ya juujuu yalikuwa mbinu mahsusi ya kuficha ushahidi.
Pia , mahakama iliiambiwa kuwa uchunguzi umekumbwa na changamoto kutokana na miili kusambazwa kwenye maeneo makubwa, kuoza vibaya na kutatizwa na wanyama, huku majukumu muhimu kama radiolojia ya uchunguzi, upasuaji maiti, upangaji wa mabaki, uchanganuzi wa DNA na uchunguzi wa uhalifu wa mtandaoni yakiwa bado yanaendelea. Mashahidi pia wametambuliwa katika kaunti tisa.
Serikali ilisema kuendelea kuwazuilia washukiwa ni muhimu kulinda ushahidi na maisha yao. “Wakiachiliwa, kuna uwezekano mkubwa watajipanga upya na kusababisha madhara zaidi,” Bw Yamina alionya, akibainisha kuwa washukiwa wengine wanane bado hawajakamatwa. Wapelelezi wameorodhesha makosa wanayochunguza kama vile kusaidia ugaidi, uhalifu wa kimfumo kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia Uhalifu Ulioandaliwa, na mauaji chini ya Kanuni ya Adhabu.
Serikali iliongeza kuwa kwa kuzingatia usalama wa kitaifa, kuna haja ya kuendesha mpango wa kuwarekebisha kimaadili, kuwatoa katika itikadi kali, kuwahusisha upya na jamii na kuwarejesha waathiriwa. Janga la Kwa Binzaro sasa linaonekana kama mwendelezo wa giza wa Shakahola, likibainisha udhaifu serikali dhidi ya misimamo mikali ya kidini