Nitashikilia kwa miezi 6 tu, kaimu waziri mkuu mpya aambia Gen Z wa Nepal
KATHMANDU, NEPAL
KAIMU Waziri Mkuu aliyeteuliwa, Sushila Karki amesema atashikilia wadhifa huo kwa miezi sita tu.
“Sikumezea mate kazi hii. Ilikuwa baada ya sauti barabarani ndipo nikalazimika kuikubali,” alisema Karki akizungumza kwa mara ya kwanza tangu alipoapishwa Ijumaa.
Alisema atakabidhi mamlaka serikali mpya itakayochaguliwa baada ya uchaguzi utakaofanyika Machi 5, mwaka ujao.
Aliteuliwa baada ya watu zaidi ya 70 kuuawa katika maandamano ya kupinga ufisadi yaliyofurusha serikali ya Nepal.
Karki alikula kiapo cha afisi baada ya maafikiano na viongozi kutoka kwa kundi linalojiita vuguvugu la “Gen Z.”
“Ni sharti tufanye kazi kuambatana na Mawazo ya kizazi cha Gen Z,” alisema.
“Kile kundi hili linadai ni ufisadi ukome, uongozi bora na usawa kiuchumi.”
Karki, aliyekuwa jaji mkuu, anachukuliwa kuwa na taswira safi.
Hata hivyo, hajakosa kuandamwa na kashfa hasa baada ya kutimuliwa katika hatamu yake ya karibu miezi 11 kama jaji mkuu.
Maandamano hayo yaliyochochewa na marufuku dhidi ya mitandao ya kijamii, yalianza Septemba 8 na katika muda wa siku mbili yakageuka vurugu na machafuko ambapo nyumba za wanasiasa ziliporwa na bunge kuteketezwa.