Kimataifa

Mshukiwa wa mauaji ya mshirika wa Trump akataa kuongea na wapelelezi

Na REUTERS September 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MSHUKIWA wa mauaji ya mwanaharakati Charlie Kirk, Tyler Robinson, amekataa kutoa maelezo kwa maafisa wa upelelezi, Gavana wa Utah Spencer Cox alisema Jumapili.

Hata hivyo, kiongozi huyo alisema wapelelezi wanashirikiana na marafiki na familia kubaini kilichomfanya Robinson, 22, kumuua Kirk kwa kumpiga risasi.

Gavana Cox, alisema kuwa mshukiwa anazuiliwa Utah na atafikishwa mahakamani Jumanne, Septemba 16, 2025.

Wapelelezi hawajapata habari kuhusu ni kwa nini Robinson alipanda kwenye paa la jengo moja katika Chuo Kikuu cha Utah Valley na kumpiga Kirk risasi shingoni Jumatano wiki jana.

Kirk, ambaye alikuwa mwandani wa Rais Donald Trump na mwanzilishi mwenza wa kikundi cha wanafunzi kwa jina “Turning Point USA” aliuawa wakati wa sherehe moja iliyohudhuriwa na zaidi ya watu 3,000 katika eneo la Orem, umbali wa kilomita 65 kutoka jiji la Salt Lake City.