Quad yafufua mazungumzo ya amani Sudan huku vita vikiendelea
HUKU vita vikali vikiendelea Sudan kwa zaidi ya mwaka mmoja mwanga wa matumaini ya kidiplomasia umeibuka huku wahusika wa kimataifa na wa kikanda wakifanya upya juhudi za kuleta amani.
Kenya, Umoja wa Afrika (AU), na Mamlaka ya Maendeleo ya Kiserikali (Igad) wameunga mkono wito wa mazungumzo mapya kati ya Jeshi la Sudan (SAF) na Vikosi vya RSF.
Wito huo ulitolewa kwa mara ya kwanza na Jumuiya ya Kimataifa ya Quad – Amerika, Saudi Arabia, Misri, na Umoja wa Falme za Kiarabu – ambayo ilitangaza ramani mpya ya kumaliza mzozo ambao umeua zaidi ya watu 40,000 na milioni 12 kukimbia makazi yao.
Kenya ilisema pendekezo hilo linaendana na msimamo wake wa muda mrefu kwamba “hakuwezi kuwa na suluhu la kijeshi kwa mzozo.”
Quad inashinikiza mazungumzo mapya mwezi Oktoba, yanayoonekana kama nafasi ya mwisho ya amani na mpito wa kiraia. Ilisisitiza kuwa umoja na uadilifu wa eneo ni jambo lisiloweza kujadiliwa, na kusisitiza kukataa suluhisho lolote la kijeshi.
Vita hivyo vimesababisha janga la kibinadamu, huku njaa ikiripotiwa huko Darfur baada ya miezi kadhaa ya kuzingirwa.
Quad ilihimiza upatikanaji wa haraka wa misaada, ulinzi wa raia, na kuzingatia Azimio la Jeddah la 2023, ambalo lilikusudiwa kuruhusu misaada na mazungumzo, lakini lilipuuzwa na pande zote mbili. Pia ilitoa wito wa kusitishwa kwa mapigano kwa muda wa miezi mitatu ili kupunguza mateso na kufungua njia ya mchakato mpana wa kisiasa.
Katika taarifa ya pamoja, AU na Igad ilisema itaitisha mashauriano na makundi ya kiraia ya Sudan mwezi Oktoba, pamoja na Umoja wa Nchi za Kiarabu, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya.
Lengo ni kuunganisha sauti za kiraia na kuandaa mazungumzo yanayoongozwa na Sudan kuelekea mpito wa kikatiba unaoongozwa na raia.
Walikaribisha mpango wa Quad, ambao unatoa wito wa kusitishwa kwa mapigano ya kibinadamu, ulinzi wa raia, mpito wa kiraia wa miezi tisa, na kupiga marufuku msaada wa kijeshi kutoka nje.