Kimataifa

WanTam yanukia Malawi Chakwera akiachwa mbali kura za urais

Na REUTERS September 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WIMBI la ‘WanTamlinaelekea kupata uhalisia Malawi baada ya matokeo ya awali kuonyesha kuwa Rais Lazarus Chakwera, 70 amebwagwa na mpinzani wake Peter Mutharika, 80.

Takwimu za awali kutoka Tume ya Uchaguzi ya Malawi zilionyesha kuwa Mutharika ambaye pia ni rais wa zamani, anaongoza kwa asilimia 60 ya kura.

Chakwera anamfuata kwa asilimia 30 ingawa nyingi za kura bado hazijahesabiwa na kudai uchaguzi huo unaweza kuingia duru ya pili.

Katiba ya Malawi inaamrisha kuwa mshindi anastahili kutangazwa katika muda wa wiki moja kwa hivyo matokeo haya huenda yakatangazwa kufikia Septemba 24.

Iwapo hakutakuwa na mshindi ambaye atapata asilimia 50 ya kura basi kutakuwa na duru ya pili ambapo mshindi na atakayeibuka wa pili watachuana tena ili rais mpya apatikane.

Tume hiyo pia inatarajiwa kutangaza matokeo ya ubunge katika muda wa siku 14 kisha uchaguzi wa madiwani ndani ya siku 21.

Wakati wa kupiga kura raia wengi wa Malawi walisema wangependa kuwa na kiongozi ambaye atasaidia kupambana na changamoto za taifa hilo hasa njaa.

Katika uchaguzi mkuu uliopita, Mutharika alimshinda Chakwera katika duru ya kwanza lakini hakufikisha asilimia 50. Uchaguzi huo ulirudiwa ambapo rais huyo wa sasa alimbwaga kwenye duru ya pili.